Na Mary Mwaisenye, Chunya.
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Chunya
mkoani Mbeya limekubaliana kupitia kuhakikisha
wanayanyang'anya makampuni yote yaliyo shikilia leseni za tafiti kwa
muda mrefu ili wachimbaji wadogo waweze kuyatumia maeneo hayo.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha
robo ya Tatu kilichofanyika jana ambapo walisema wachimbaji wadogo wadogo
wa madini ya dhahabu wamekuwa wakinyanyaswa na wachimbaji ambao
wamekuwa wakishika leseni bila kuyatumia maeneo waliyopewa.
Akizungumza katika kikao hicho mbunge wa jimbo la Lupa
Victor Mwambalaswa, alisema hawezi kuona wachimbaji wadogo wadogo
wilayani kwake wakiwa wananyanyaswa na wachimbaji wakubwa ambao wamekuwa
wakishikiria leseni kwa muda mrefu bila kuzitumia na kusubiri mchimbaji
mdogo avumbue maeneo yenye dhahabu ndipo wanajitokeza na kusema ni maeneo yao.
Alisema yeye kama kiongozi atahakikisha anamshauri waziri
mwenye dhamana kuhakikisha wale walioshikiria maeneo hayo kuazia mwaka
2005 hadi sasa wanawaachia wachimbaji wadogo ili waweze kuyatumia ili
kuepusha migogoro kati ya wachimbaji wadogo kwa wakubwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Chunya Noeli
Chiwanga alisema kuna haja ya serikali kuu kuhakikisha wanawatazama
wachimbaji wadogo kwa jicho la tatu kutokana na kwamba wao ndio walioko
maeneo husika na ndio wavumbuzi wakubwa wa maeneo hayo yalio na leseni
lakini wanapochimba wanaambiwa eneo hilo lina leseni na mwenye leseni
yuko Dar es salaam na wachimbaji wadogo kufukuzwa.
Chiwanga alisema kama mwenyekiti wa chama hafurahishwi
kabisa na wachimbaji wadogo kufukuzwa katika maeneo ambayo wamekuwa
wakiyavumbua hivyo anakubaliana na maamuzi ya baraza hilo la Madiwani kuazimia leseni za
muda mrefu kufutwa.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Halmshauri Bosco
Mwanginde alisema kama baraza lazima waungane kwa pamoja katika
kusimamia sheria na mipango yote inayowekwa baraza lao ili kuhakikisha
maendeleo ya halmshauri yanasonga mbele.
Mwanginde alisema pamoja na kuiomba serikali kuu
kuzifuta leseni za muda na kupewa wachimbaji wadogo wadogo pia aliomba
madiwani kuhakikisha wanawaelimisha wachimbaji wadogo wadogo kuhusiana
na tozo zilizowekwa na Halmshauri ili waone kulipa tozo hizo ni uzalendo
katika kujenga wilaya yao.
Mwanginde pia alisisitiza madiwani kusimamia watendaji wa
kata na vijiji kusimamia mapato hasa katika kipindi hiki cha mavuno
ili waweze kukamilisha vyema robo iliyobakia ambapo alisema kwa sasa
wamefikia 73%.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Rehema Madusa akiwasilisha
salamu zake kwa madiwani aliwataka watendaji wa halmshauri kuwa wabunifu
wa vyanzo vya mapato ili kuongeza mapato ya Halmshauri na kufikia
malengo yaliyowekwa na Serikali kuu.




No comments:
Post a Comment