Na Gordon Kalulunga, Mbeya

NCHI mbalimbali duniani zimejipanga kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, maarufu kama COP30, unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho Novemba 10,2025 mjini Belém, Brazil.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kutumia mkutano huo kuwasilisha ajenda yake kuhusu nishati safi, mazingira, na maendeleo endelevu.

Mkutano wa COP30 ni mkutano wa thelathini wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi – UNFCCC.

Mkutano huu unakusudia kutathmini hatua ambazo dunia imepiga katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuweka mikakati mipya ya kulinda mazingira.

Kwa mwaka huu, mazungumzo yataangazia utekelezaji wa makubaliano ya Paris, ufadhili wa miradi ya tabianchi, na kuharakisha mabadiliko kuelekea nishati safi kama suluhisho la kupunguza hewa ukaa.

Kwa upande wa Tanzania, serikali inatarajia kutumia jukwaa hilo kuhimiza ufadhili na ushirikiano katika sekta ya nishati safi, hususan miradi ya gesi asilia, umeme wa jua na matumizi ya majiko banifu.

“Kupitia COP30, tunatarajia kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi na kuhakikisha kaya nyingi nchini zinatumia nishati rafiki kwa mazingira.”

Tanzania pia itawasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa Nationally Determined Contributions (NDCs) – ikilenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa zaidi ya asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, nchi inatarajia kupata ufadhili wa kimataifa kusaidia miradi ya upandaji miti, uhifadhi wa misitu, na uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa jua vijijini.

Wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la mabadiliko ya tabianchi, Tanzania inaiona COP30 kama fursa ya kuchochea uchumi wa kijani na kukuza ajira kupitia sekta ya nishati safi.

Huo ulikuwa mwangwi wa Tanzania kuelekea mkutano wa COP30 unaotarajiwa kufanyika Brazil.