Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zimeingia mkataba wa mashirikiano ya kimkakati yenye lengo la kukuza Utalii wa Tiba nchini pamoja na kuongeza thamani ya mazao mengine ya utalii.
Katika kikao kilichowahusisha viongozi wa juu wa taasisi hizo, Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Peter Kisenge na Ephraim Mafuru wa TTB, pande zote mbili zimekubaliana kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha huduma za kibingwa za afya kwa wageni kutoka ndani ya ukanda wa Afrika na mataifa mengine duniani.
Mkakati huo unajumuisha kuimarisha na kuzitangaza huduma za uokoaji na matibabu ya dharura katika maeneo ya vivutio vya utalii, mikusanyiko mikubwa ya wageni, pamoja na matukio ya kimataifa yanayofanyika nchini. Kupitia mpango huu, Tanzania itatangazwa kama kituo salama ambacho mtalii anaweza kupata huduma za kibingwa za afya wakati wowote anapohitaji akiwa katika ziara zake za kitalii.
Ili kufanikisha azma hiyo, Bodi ya Utalii imeishauri JKCI kushiriki kikamilifu katika majukwaa makubwa ya kimataifa ikiwemo maonesho ya Swahili International Tourism Expo (SITE) na Meetings Africa.
Kushiriki katika majukwaa haya kutaipa Tanzania nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika kutoa huduma za matibabu ya moyo, ikizingatiwa kuwa JKCI ni miongoni mwa taasisi tatu bora barani Afrika kutokana na ubora wa vifaa tiba na weledi wa wataalamu wake.
Ushirikiano huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa kwa kuunganisha sekta ya afya na utalii, jambo ambalo litaongeza idadi ya wageni wanaokuja nchini kwa malengo ya kupata matibabu na kisha kutembelea vivutio vya asili.
Hatua hii inalenga kuliweka taifa mbele zaidi katika ushindani wa soko la kimataifa la utalii wa tiba, huku ikihakikisha kuwa Tanzania inatambulika kama kimbilio la huduma bora za kibingwa barani Afrika.

0 Comments