Kwa miaka mingi, kijana wa Kitanzania amekuwa akiamini kuwa utajiri unapatikana tu kwa kukaa kwenye kiti cha ofisini au kulima ardhi kwa jembe la mkono. Lakini simulizi linabadilika; sasa "shamba" limehamia baharini. Kupitia ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Korea Kusini, uvuvi unakuwa siyo tena kazi ya kusubiri bahati au kupambana na mawimbi bila mwelekeo, bali ni uwekezaji wa kisayansi unaotumia macho ya satelaiti kutoka angani.
Kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea Kusini mnamo Mei 2024, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeingia kwenye ukurasa mpya, wakiimarisha uwezoi wa vijana kushughulika na uvuvi baharini kwa nguvu kubwa. Kupitia taasisi ya TAFIRI na KIOST ya Korea, wataalamu na vijana wa Kitanzania sasa wanapikwa kutumia teknolojia ya satelaiti ambayo inafanya uvuvi kuwa na tija zaidi.
Kazi siyo Suti, Kazi ni Bahari
Mkurugenzi wa TAFIRI, Ismael Kimirei, anasisitiza kuwa huu ni wakati wa vijana kuacha kuchoka na maisha ya mitaani wakisubiri ajira za "white collar." na kushiriki katika mradi huu wa miaka minne ambao unatoa mafunzo na unawaandaa vijana kwenda Korea Kusini kupata ujuzi zaidi utakaowageuza kuwa mabingwa wa uchumi wa buluu.
Badala ya kulalamika kuhusu ajira na kipato, kwa kujua teknolojia hii kunawapa uwezo wa kuwa wajasiriamali wa uvuvi wasiobahatisha.
Mtafiti Keunyong Kim kutoka Korea akizungumza kwenye mafunzo ya matumizi ya teknolojia hiyo ya setelaiti amewasihi vijana kuacha mzaha na kujifunza kwa bidii teknolojia hiyo kwani ni silaha ya kuua umaskini.
Kwa vijana dunia imebadilika wanapaswa kutambua kwamba tajiri wa sasa hategemei tu nguvu ya misuli, bali anatumia data za satelaiti kuvuna mabilioni yaliyofichwa chini ya maji ya Bahari ya Hindi.
Hii ndilo "shamba" jipya la Tanzania bahari inasubiri ivunwe kisasa na vijana ndio wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa maarifa zaidi.
Kwa kutumia teknolojia ya satelaiti wavuvi watatambua kirahisi na bila kubahatisha mazalia ya samaki: satelaiti inawawezesha wavuvi kujua mahali hasa walipo samaki wengi, hivyo kuokoa muda na mafuta ya boti badala ya kuzunguka bahari nzima bila mafanikio.
Pia teknolojia hii inasaidia kufuatilia mienendo ya maji na mazingira ya bahari ili kuzuia uvuvi haramu na kuhakikisha samaki hawatoweki kwa ajili ya vizazi vijavyo huku ikitoa taarifa za hali ya hewa na mawimbi kwa usahihi, jambo linalomhakikishia mvuvi usalama wake anapokuwa "shambani."
0 Comments