Jiji la Dar es Salaam Februari 8 lilikuwa na shamrashamra za kihistoria kwani baada ya kusubiri kwa hamu, hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Soko Kuu la Kariakoo lililofanyiwa maboresho makubwa na ujenzi wa soko jipya la kisasa lenye ghorofa sita.
Kumbukumbu ya Julai 10, 2021, ambapo soko la zamani liliungua na kuteketeza mitaji ya wanyonge, sasa imefutwa na majengo haya ya kifahari ambayo Rais amesema yanapaswa kuwa mfano kwa Afrika nzima.
Rais Samia hakuishia tu kuzindua majengo, bali aligusa mambo yanayomgusa mwananchi moja kwa moja:
Aidha kwa mara ya kwanza, soko limepewa sura ya utu! Rais ameagiza kuwe na maeneo ya kunyonyeshea na kulelea watoto (Day Care). Hii inamaanisha mama anaweza kufanya biashara yake kwa amani huku mwanae akiwa salama.
Pia kuonesha ni kwa namna gani serikali yake inajali kila mtanzania kujipatia riziki halali, ameagiza viongozi kuweka utaratibu maalum wa maegesho na njia za kupita bodaboda na maguta ili nao wapate fursa ya kipato ndani ya soko hilo bila usumbufu.
Rais Samia pia ameagiza TAMISEMI kuhakikisha wale wafanyabiashara waliokuwepo mwanzo wanarudi kwenye maeneo yao bila kujuana, upendeleo, wala wakubwa kuhodhi vizimba na kuwakodishia masikini kwa bei juu.
Kwa ujumla Rais akitaka Kariakoo iwe kitovu cha biashara kwa nchi jirani (DRC, Zambia, Malawi, nk) ameagiza uwapo wa mfumo ambapo mtu akinunua mzigo wake Kariakoo, mawakala wa kusafirisha mizigo nje ya nchi wawepo hapohapo sokoni. Unanunua, unapack, unasafirisha—yote sehemu moja!. Ili kurahisisha maisha ameagiza kuwepo kwa huduma za fedha na mabenki huku akitaka bidhaa zitakazouzwa zitakuwa na ubora wa hali ya juu ili kulinda jina la Tanzania kimataifa.
Rais alisisitiza kuwa miundombinu ya zimamoto iliyowekwa isibaki kuwa mapambo. Ameagiza wafanyabiashara wote wapewe mafunzo ya jinsi ya kutumia vifaa vya kuzima moto ili majanga ya nyuma yasijirudie.
Katika mkutano wake huo akizundua soko hilo pia amesema ahadi yake ya kujenga soko la Jangwani iko palepale na ujenzi utaanza mara tu daraja la Jangwani litakaponyanyuka kidogo.
Uzinduzi wa soko hili ni ushahidi kuwa Rais Samia anajali uchumi wa wananchi wanyonge. Soko hili si kwa ajili ya wenye nacho tu, bali ni uwanja wa kila Mtanzania mwenye ndoto ya kujikwamua kimaisha. Kariakoo sasa ni zaidi ya soko; ni heshima ya Taifa!

0 Comments