Mama Samia afikisha teknolojia vijijini kuwezesha tehama

Serikali imedhamiria kuimarisha ufikishaji wa taarifa vijijini kwa kutumia fursa za mawasiliano ya kidijitali, hatua inayolenga kuhama kutoka mfumo wa kizamani wa kutoa taarifa bila majibu kwenda mfumo wa kimijadala zaidi. 

Katika wasilisho la Mh. Rodney T. Mbuya mnamo Februari 13, 2026, kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa utangazaji 2026 ameeleza kuwa mawasiliano sasa ni mchakato wa kubadilishana mawazo na hisia kati ya serikali na wananchi. 

Takwimu mpya zinaonesha ukuaji mkubwa wa teknolojia, ambapo usajili wa laini za simu nchini umefikia milioni 106.9 kufikia Desemba 2025, huku matumizi ya intaneti yakipanda kwa asilimia 9.5 ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu. Kwa sasa, WhatsApp inaongoza kwa kuwa na watumiaji milioni 9.9, ikifuatiwa na Facebook (milioni 8.38) na Instagram (milioni 3.7), jambo linalofanya majukwaa haya kuwa kiungo muhimu kati ya viongozi na wapiga kura wao.

Ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia watu wa vijijini, serikali imeshatekeleza mradi wa "Tanzania ya Kidijitali" uliokamilisha ujenzi wa minara 758 katika kata zote 713, hali iliyonufaisha wananchi milioni 8.5. 

Aidha, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ujenzi wa minara mingine 201 unaendelea katika mikoa 29 ili kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 2.7. 

Serikali pia imeweka mazingira wezeshi kwa kushusha viwango vya ada kwa wamiliki wa vyombo vya habari vya mtandaoni na kuhakikisha umeme unafika katika kila kitongoji ili vifaa vya mawasiliano viwe na uhakika wa kufanya kazi. 

Pamoja na kasi hiyo ya kidijitali, Rodney Mbuya amesisitiza kuwa vyombo vya habari vya asili kama Radio, TV na Magazeti bado ni muhimu sana, hivyo kuna haja ya kuimarisha uhusiano kati ya serikali na waandishi wa habari ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, na kupunguza mianya ya rushwa.

Post a Comment

0 Comments