Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewasihi watu wenye uwezo kuwatunza wazazi na ndugu ili kuenzi mchango wao katika jamii.
Mhandisi Mahundi amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea makazi ya wazee yanayomilikiwa na taasisi binafsi ya Tushikamane Pamoja Foundation,Kwembe, Manispaa ya Ubungo Jijini Dar Es Salaam ambapo amesema jamii inapaswa kubadili mtazamo na kuhakikisha wazee wanapewa upendo, ulinzi na matunzo wanayostahili bila kujali changamoto zilizopita.
Ameeleza kwamba hata kama walipitia changamoto au walikosewa, ni muhimu kulipa kwa wema na si kwa mabaya, kwa sababu wazee ni tunu ya taifa na wana mchango mkubwa katika malezi na ujenzi wa jamii yetu.
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wanaojitoa kuwahudumia wazee ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki na wanaendelea kuishi kwa heshima na usalama,
Awali, akisoma taarifa fupi ya kituo hicho Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dkt. Aristides Raphael, , amesema Serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na uongozi wa makazi hayo ambapo imefanikisha kuwapatia wazee wote bima za afya, Afisa Ustawi wa Jamii anayefika kituoni hapo mara mbili kwa wiki kwa ajili ya uangalizi na ushauri, pamoja na madaktari wanaotoa huduma za matibabu na huduma nyingine muhimu.
“Ushirikiano huu umewezesha wazee hawa kupata huduma muhimu ikiwemo matibabu, ufuatiliaji wa afya zao pamoja na ushauri wa kijamii, jambo ambalo limechangia kuboresha hali yao ya maisha na kuwafanya waishi kwa matumaini na utulivu zaidi,” amesema Dkt. Aristides.
Kwa upande wao, baadhi ya wazee wanaoishi katika makazi hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na kuthamini ustawi wao
wakieleza kuwa ujio wa viongozi na misaada mbalimbali imekuwa faraja kubwa kwao na uthibitisho kuwa bado wanatambuliwa na kuthaminiwa katika jamii.
“Tunashukuru Serikali na wadau mbalimbali kwa kuendelea kutupa faraja na kututembelea. Hii inatupa furaha kubwa na kutufanya tuone bado tuna thamani katika jamii. Tunaamini kweli kuwa wazee ni tunu ya Taifa na tunaomba juhudi hizi ziendelee ili kuwasaidia hata wazee wengine wenye uhitaji,” amesema mmoja wa wazee hao.
Makazi hayo yamekuwa yakitoa huduma za malezi, malazi na uangalizi kwa wazee wenye uhitaji, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kundi hilo linapata haki, heshima na ustawi unaostahili.





0 Comments