SERIKALI ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetuma salamu nzito kwa watendaji wa umma wanaozembea kutoa haki za wananchi baada ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuamuru watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuchanga fedha mifukoni mwao kumlipa papo hapo mwananchi aliyekuwa akidai tangu mwaka 2022.
Tukio hilo la kushtukiza limetokea jana, Februari 18, 2026, katika mkutano wa hadhara eneo la Ndungu, baada ya mkandarasi mmoja wa kizawa kujitokeza mbele ya Waziri Mkuu na kueleza masahibu yaliyompata kutokana na ucheleweshaji wa malipo yake ya ujenzi wa matundu ya vyoo vya shule.
Akizungumza kwa uchungu mbele ya umati wa wananchi, mkandarasi huyo alieleza kuwa deni hilo la Shilingi milioni mbili limemletea athari kubwa za kijamii na kiuchumi. Alibainisha kuwa kutolipwa kwake kulisababisha kupoteza baadhi ya mali zake, mgogoro mkubwa wa ndoa uliotishia familia yake, na kushindwa kuwalipa vibarua waliomsaidia kazi hiyo tangu miaka minne iliyopita.
Simulizi hiyo ya kuhuzunisha ilionekana kumgusa Waziri Mkuu ambaye hakusubiri maelezo marefu ya kiofisi, bali aliamua kuchukua hatua ya papo kwa hapo ili kurejesha heshima ya mwananchi huyo na serikali kwa ujumla.
Dkt. Mwigulu, kwa sauti ya mamlaka, aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo wanaohusika na mchakato wa malipo hayo "kujitathmini" kama wanastahili kuendelea na nafasi zao ikiwa jambo dogo kama hilo linamtesa mwananchi kwa miaka minne. Aliagiza watendaji hao kuchangishana kiasi hicho cha fedha na kumkabidhi mwananchi huyo mbele ya mkutano, akisisitiza kuwa Serikali ya Samia haina urafiki na watendaji wanaovuruga ustawi wa wananchi.
"Hatuwezi kuwa na watendaji wanaokaa ofisini huku wananchi wakiteseka kwa madeni ya tangu 2022. Kama fedha zipo na mchakato ulikamilika, kwanini asilipwe? Kama hamuwezi kumlipa kwa taratibu za ofisi mlizozikwamisha, lipeni hapa hapa," kilisikika chanzo kimoja kikikariri msisitizo wa kiongozi huyo.
Tukio hili limeibua mijadala mipana miongoni mwa wananchi na wachambuzi wa masuala ya utawala. Wengi wamepongeza hatua hiyo wakisema inarudisha nidhamu ya kazi serikalini. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wametoa rai kuwa mifumo ya halmashauri inapaswa kujiendesha kwa ufanisi bila kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa.
Msimamo huu wa Dkt. Mwigulu ni kielelezo tosha kuwa kaulimbiu ya "Kazi Iendelee" inaambatana na "Haki kwa Wote." Inapeleka ujumbe kwa wakurugenzi, wahasibu, na wahandisi wa wilaya nchi nzima kuwa uzembe, urasimu, na dharau kwa madai ya watoa huduma wadogo hautavumiliwa tena.
Baadhi ya wananchi waliokuwepo mkutanoni walionekana kushangilia hatua hiyo wakisema ni "maamuzi ya kiume" na yenye tija. "Huu ndio utaratibu tunaoutaka. Mwananchi amefanya kazi, apewe haki yake. Serikali ya Mama Samia inaonyesha kuwa haiko mbali na watu wa chini," alisema mmoja wa wakazi wa Ndungu.
Kwa hatua hii, Serikali imethibitisha kuwa mtendaji yeyote atakayeshindwa kwenda na kasi ya Rais Samia katika kuwahudumia wananchi, hana budi "kukaa pembeni" ili kupisha damu ngeni yenye uchungu na matatizo ya watu.

0 Comments