TANZANIA YA SAMIA: KISIWA CHA MATUMAINI KINACHOPAA WAPOTOSHAJI WAZAMA KWENYE TOBO LA UZUSHI

Katika kipindi hiki ambacho dunia inaitazama Tanzania kwa matumaini makubwa kutokana na hatua kubwa za kimaendeleo zinazopigwa, Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha uongozi thabiti kwa kuifanya nchi kuwa kitovu cha diplomasia na uwekezaji wa kimkakati. 

Kupitia mfululizo wa mikutano ya ngazi ya juu iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesisitiza dhamira ya serikali yake ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaoakisi Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, huku akionyesha kuwa licha ya uvumi na uzushi unaoweza kusambazwa mitandaoni kwa lengo la kufadhaisha umma, ukweli wa mwelekeo wa nchi upo katika matokeo chanya ya kidiplomasia na kiuchumi yanayomulika ulimwenguni.

Ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore unatajwa kuwa moja ya nguzo muhimu katika safari hii ya mageuzi, ambapo katika mazungumzo na Balozi Douglas Foo, Rais Samia amebainisha nia ya kujifunza kutoka kwa nchi hiyo katika ujenzi wa taasisi imara na kukuza wajasiriamali vijana.

Lengo kuu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ushindani wa biashara duniani kwa kuimarisha sekta za teknolojia, elimu, na miundombinu ya kisasa. Vipaumbele vya Dira 2050 vimejikita katika mabadiliko ya kidijiti na kuongeza thamani kwenye sekta ya kilimo ili kuhakikisha tija na ushindani wa uchumi wetu unapaa kimataifa.

Katika nyanja ya utawala bora na demokrasia, Rais Samia amepokea pongezi za kipekee kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Martin Chungong, kwa mafanikio makubwa ya Tanzania katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia na utawala shirikishi. 

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa IPU utakaofanyika Arusha Oktoba 2026, ukiwa na wageni zaidi ya 2,000, ni kielelezo tosha cha imani ambayo jumuiya ya kimataifa inayo kwa Tanzania kama kisiwa cha utulivu na ukarimu. Mkutano huu unatarajiwa kutoa taswira halisi ya maendeleo ya nchi na kuzima kelele za upotoshaji zinazoweza kuwepo.

Sekta ya afya pia imepata msukumo mpya baada ya Rais Samia kukutana na ujumbe wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ukiongozwa na Profesa Mohamed Janabi, ambapo jitihada za Tanzania katika kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote na kuboresha afya ya mama na mtoto zimepongezwa sana. 

Rais amesisitiza umuhimu wa tafiti zaidi katika kukabiliana na changamoto za kiafya, huku akishukuru WHO kwa ushirikiano wao. Hatua hizi zote za kimkakati zinathibitisha kuwa Rais Samia anaivusha Tanzania kuelekea eneo sahihi la ustawi, usalama wa afya, na ukuaji wa kiuchumi usioyumba.


Post a Comment

0 Comments