TUJIFUNZE KWA VIJANA WA MAKUNDUCHI WALIOGEUZA TAARABU ASILIA KUWA ‘MIGODI’ YA FEDHA MTANDAONI


Wakati baadhi ya vijana wakiendelea kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira rasmi, kundi la vijana wanane kutoka Kijiji cha Makunduchi, Kusini Unguja, limeibuka na jibu la vitendo: Ubunifu ndio ajira ya kisasa.

Vijana hao, wakiongozwa na kijana mtanashati Ibrahim Suleiman, wameamua kutumia muziki wa Taarabu asilia—urithi ambao wengi waliuona kama kitu cha kizamani—na kuugeuza kuwa bidhaa adimu inayouzika kupitia mitandao ya kijamii. Wao badala ya kusubiri majukwaa makubwa, wameamua kutumia simu zao za mkononi kutengeneza maudhui yanayochanganya vichekesho na midundo ya jadi, jambo lililowafanya kuwa gumzo kote nchini na nje ya mipaka.

“Tumeamua kutumia kile tulichonacho mkononi. Hatukusubiri kuajiriwa, tuliamua kujiajiri kupitia kipaji chetu na utamaduni wetu,” anasema Ibrahim Suleiman, akisisitiza kuwa soko la sasa linataka kitu cha kipekee (Originality).

Ubunifu wa vijana hawa si tu unawaingizia kipato kupitia watazamaji wa mtandaoni (views) na matangazo, bali pia unalinda heshima ya muziki wa jadi wa Zanzibar usipotee. 

Hii ni dhihirisho tosha kwa vijana wengine wa Kitanzania kuwa; uwe una ujuzi wa VETA, unalima parachichi, au unajua kuimba, nguvu ya kugeuza ujuzi kuwa utajiri iko kwenye ubunifu wako na matumizi sahihi ya teknolojia.

Huu ni ujumbe mzito kwa wale wanaopoteza muda kubeza juhudi za maendeleo: Wakati ninyi mkiandika vibaya mitandaoni, wenzenu wa Makunduchi wanatumia mitandao hiyo hiyo kuvuna fedha na kutangaza utamaduni wa nchi yao. Tanzania ya sasa inahitaji vijana wenye "misuli ya akili" kama hawa, wanaoona fursa pale wengine wanapoona matatizo.

Post a Comment

0 Comments