UMOJA NA AMANI: Nguzo Kuu ya Mageuzi ya Kiuchumi


Mafanikio makubwa ya kiuchumi yanayoshuhudiwa nchini kwa sasa, ikiwemo kuongezeka kwa meli za kitalii mkoani Lindi na kutanuka kwa fursa za ajira kwa vijana, yametajwa kuwa ni matunda ya misingi imara ya amani na mshikamano iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Hayo yamebainishwa na wadau mbalimbali mkoani Simiyu, ambao wamesisitiza kuwa kuepuka "sumu" ya udini na ukabila si tu jukumu la kijamii, bali ni hitaji la lazima la kiuchumi. Wameeleza kuwa mazingira ya amani ndiyo sumaku inayovuta wawekezaji na watalii ambao ni kiungo muhimu katika kukuza pato la taifa.

Akizungumzia umuhimu wa utulivu, Shehe Issa Masanja, mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, alieleza jinsi ukosefu wa amani unavyoweza kuathiri hadi uhuru wa kuabudu na mahusiano ya mwanadamu na Muumba wake.

"Suala la amani na umoja lina umuhimu mkubwa sana. Tumeona mitihani ambayo kama taifa tuliipata ikaleta taharuki kubwa. Hata kwetu watu wa dini ilituletea shida, hadi kufikia hatua ibada za usiku tukawa hatufanyi. Amani ni kitu cha muhimu katika kujenga mahusiano mazuri na Mungu kupitia ibada," alisema Shehe Masanja.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Bariadi, Musa Mseti, alisisitiza kuwa amani ndiyo uti wa mgongo wa kila jambo zuri linalofanyika nchini, akionya kuwa taharuki yoyote hupoteza mwelekeo wa nchi.

"Amani ndiyo kila kitu. Vyote tunavyoona vinafanyika vizuri ni kwa sababu amani haijatoweka. Tumejionea yaliyotokea huko nyuma, kila mtu alitaharuki. Kuwepo kwa amani kuna maana kubwa sana kwa taifa letu," alieleza Mseti.

Naye mjasiriamali wa Bariadi, Hamis Omary, aligusia upande wa kisaikolojia wa amani, akibainisha kuwa utulivu wa nchi unampa mwananchi hamasa ya kufanya kazi kwa bidii na kujiamini katika mazingira yoyote.

"Amani inakufanya uwe na hamasa kubwa na kujiamini katika sehemu yoyote ile uliyopo. Pia, amani ina maana ya kurudi kwa Mungu wako pindi unapoona umekosea na kufanya maamuzi tofauti," alisema Omary.

Wakati vijana nchini wakihimizwa kuchangamkia fursa tele zilizopo kwenye sekta ya utalii na ujasiriamali, wamekumbushwa kuwa wajibu wao wa kwanza ni kulinda umoja wa kitaifa uliodumu kwa zaidi ya miongo sita.

Msisitizo umetolewa kuwa ushindani wa kisiasa unapaswa kubaki kwenye hoja, sera, na ajenda za maendeleo, huku amani ikisalia kuwa msingi mkuu na usiojadiliwa kwa ajili ya ustawi wa kudumu wa Tanzania

Post a Comment

0 Comments