VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA TISEZA, WAACHE CHUKI MITANDAONI

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetoa wito kwa vijana nchini kuacha kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii kwa kufuatilia mambo ya upuuzi na chuki, badala yake watumie muda huo kutafuta fursa za kiuchumi zinazotolewa na mamlaka hiyo. 

Wito huo umetolewa jijini Mbeya wakati wa ziara ya mamlaka hiyo katika kiwanda cha vinywaji changamshi cha Mati Dry Gin, kinachomilikiwa na kampuni ya Kitanzania ya Mati Group of Companies Limited iliyopo eneo la Iwambi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, Daudi Riganda, amesisitiza kuwa amani iliyopo nchini ndiyo inayotoa mwanya wa uwekezaji, hivyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuilinda badala ya kuitumia mitandao vibaya. 

Alibainisha kuwa uwekezaji wa ndani una mchango mkubwa katika kutoa ajira na kukuza uchumi, jambo ambalo haliwezi kufikiwa ikiwa jamii itakumbatia chuki na vurugu zinazochochewa kidijitali.

Kwa upande wake, Meneja wa Fedha wa Mati Group, Davis Bila, akimwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alisema kiwanda chao kilianza uzalishaji Februari 2, 2023, kwa mtaji wa shilingi milioni 500 na mpaka sasa kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 55. 

Alieleza kuwa usajili wao kupitia TISEZA umewapa manufaa makubwa, ikiwemo unafuu wa ushuru wa forodha kwa asilimia 75 pamoja na urahisi wa kupata nyaraka muhimu za uwekezaji.

Serikali imeendelea kuwahimiza Watanzania kuiga mfano wa kampuni ya Mati Group kwa kuwekeza katika sekta za uzalishaji. Ujumbe mkuu unabaki kuwa: amani ni silaha na mtaji, na vijana wanapaswa kutambua kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana kwa kufanya kazi na kutumia fursa kama za TISEZA, huku wakidumisha umoja wa kitaifa kwa kauli mbiu ya "Tanzania Kwanza."

Post a Comment

0 Comments