AMANI YAFUNGUA MILANGO: TANZANIA NA DRC KUFANYA BIASHARA KUBWA YA MAHINDI

Wakati amani na utulivu vikiendelea kushika kasi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ziko katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya biashara ya mahindi.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya kikazi ya maafisa wa Serikali ya DRC, wakiongozwa na Tony Bandio Munongoll kutoka Ofisi ya Rais wa nchi hiyo, ambao  Machi 12, 2026, ambapo walikagua maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yaliyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi  NFRA, Balozi John Ulanga, amesema ujio wa ujumbe huo ni matokeo ya mazungumzo ya awali yaliyofanywa na ujumbe wa Tanzania nchini DRC. Alibainisha kuwa kuwepo kwa amani kumeruhusu nchi hizi mbili kushirikiana kimkakati katika kuhakikisha usalama wa chakula unapatikana kwa pande zote.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba, amewahakikishia Watanzania kuwa biashara hiyo haitaathiri akiba ya ndani. Alifafanua kuwa NFRA tayari imehifadhi kiasi cha kutosheleza mahitaji ya nchi endapo kutatokea dharura, na kile kinachozungumzwa kuuzwa DRC ni ziada iliyopatikana.

"NFRA ina jukumu mama la kuhakikisha nchi ina chakula cha kutosha. Kiwango hicho tayari kipo, na kile kinachouzwa sasa ni ziada ambayo imeongezeka kwenye akiba yetu," alisema Dkt. Komba.

Wataalamu wa uchumi wanabainisha kuwa biashara hii siyo tu itaiingizia Tanzania fedha za kigeni, bali pia ni ushahidi kuwa mazingira bora ya amani yanaruhusu Serikali kufanya shughuli zake na wananchi kunufaika na jasho lao kupitia kilimo cha biashara.

Ziara hiyo ya maafisa wa DRC imekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania imekuwa ikijipambanua kama "ghala la chakula" kwa nchi jirani, jambo linalowezekana kutokana na sera thabiti za kilimo na usimamizi madhubuti wa rasilimali.

Post a Comment

0 Comments