Serikali imetoa onyo kali dhidi ya waajiri wanaokiuka sheria za kazi nchini baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, kuipa Kampuni ya Tabono Consultant muda wa siku saba kufika ofisini kwake jijini Dodoma.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ripoti ya ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Sumbawanga (TAZA), unaosimamiwa na kampuni ya TBEA Co Ltd, ambapo kampuni ya Tabono inatuhumiwa kudhulumu haki za msingi za wafanyakazi wake.
Katika kile kinachoonekana kama hujuma dhidi ya ujira wa wafanyakazi, kampuni hiyo inatuhumiwa kukata fedha za michango ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutoka kwenye mishahara ya watumishi lakini kutoziwasilisha katika mamlaka husika.
Kitendo hiki si tu kinahujumu maisha ya baadae ya mfanyakazi, bali kinamnyima haki ya kupata fidia pindi anapopata ajali au ugonjwa uliotokana na kazi, jambo ambalo serikali imesisitiza kuwa halitavumiliwa hata kidogo.
Aidha, Waziri Sangu ameelekeza uongozi wa kampuni hiyo kufika mbele ya Kamishna wa Kazi ukiwa na nyaraka zote za usajili ili kubaini uhalali wao kisheria, kufuatia taarifa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi kama mwajiri na wakala wa ajira kwa wakati mmoja kinyume na taratibu.
Vilevile, kampuni hiyo imetakiwa kuwasilisha ripoti ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na maelezo ya kina kuhusu malalamiko ya kukatisha mikataba ya wafanyakazi kiholela, jambo ambalo linatishia usalama wa ajira kwa wazawa wanaofanya kazi katika miradi ya kimkakati.
Msimamo huu wa serikali unadhihirisha dhamira ya dhati ya kulinda 'Ajira na Ujira' kwa kuhakikisha kuwa kila mwekezaji au mkandarasi anafuata Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. Kwa kuingilia kati mradi wa TAZA mkoani Rukwa, Waziri Sangu ametuma ujumbe mzito kwa waajiri wote nchini kuwa, kigezo cha kuwa mgeni katika nafasi ya uongozi—kama alivyojitetea Ofisa Rasilimali Watu wa Tabono—hakiondoi wajibu wa kampuni kulipa madeni na mafao ya wafanyakazi wake kwa wakati.
Hatua hii ya serikali imepokelewa kama ngao kwa wafanyakazi wanyonge, ikionyesha kuwa jasho la Mtanzania linalindwa na vyombo vya dola. Kupitia usimamizi huu wa karibu, serikali inalenga kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kitaifa haileti tu miundombinu, bali inajenga ustawi wa kiuchumi kwa wafanyakazi kupitia mishahara ya haki, hifadhi ya jamii ya uhakika, na mazingira salama ya kazi yanayozingatia utu na sheria za nchi.
0 Comments