MAHUNDI ATOA MIL. 5 KUUNGA MKONO UJENZI SHULE YA SEKONDARI BAKWATA MBEYA


Mbeya

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya kupitia kundi la wanawake, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ametembelea ofisi za BAKWATA Mkoa wa Mbeya na kukabidhi shilingi milioni tano, kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya BAKWATA Mkoani humo.

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni mbili zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi ikiwemo nondo na saruji, huku shilingi milioni tatu zikitolewa taslimu kusaidia kuendeleza ujenzi wa shule hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mhe. Mahundi amesema ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta rasilimali zaidi ili kuharakisha ujenzi wa shule hiyo muhimu kwa jamii.

“Elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii. Nitaendelea kutafuta wadau na washirika ili tuongeze nguvu katika kukamilisha ujenzi wa shule hii ambayo itawanufaisha vijana wengi wa Mkoa wa Mbeya,” amesema Mhe. Mahundi.

Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa BAKWATA Mkoa wa Mbeya Ndg.Ayas Njalambaah  amesema shule hiyo haitawahudumia Waislamu pekee bali itakuwa wazi kwa wanafunzi wa dini zote, kwa lengo la kuimarisha elimu na mshikamano wa jamii.

Aidha, amempongeza Mhe. Mahundi kwa moyo wake wa kujitolea katika maendeleo ya taasisi hiyo, akibainisha kuwa hata katika ujenzi wa ofisi za BAKWATA mkoa wa Mbeya, fedha za kuweka jiwe la kwanza zilitolewa na Mhe. Mahundi mwenyewe.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mahundi kwa moyo wake wa kujitoa. Ameendelea kuwa sehemu ya maendeleo ya taasisi yetu tangu mwanzo, ikiwemo kufanikisha hatua za awali za ujenzi wa ofisi hizi,” amesema Sheikh huyo.


Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya BAKWATA Mkoa wa Mbeya unatarajiwa kusaidia kuongeza fursa za elimu kwa vijana na kuchochea maendeleo ya elimu katika eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments