Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Sikukuu ya Eid lililofanyika jijini Mbeya.
Baraza hilo limefanyika katika ukumbi wa City Garden, likiwakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo kusherehekea sikukuu ya Eid kwa pamoja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Mahundi amewapongeza waumini wa Kiislamu kwa kumaliza mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwataka kuendelea kudumisha amani, mshikamano na upendo katika jamii.
Amesema serikali inaendelea kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika kuimarisha maadili mema na umoja wa kitaifa, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuleta maendeleo endelevu.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa dini wameeleza kufurahishwa na ushiriki wa viongozi wa serikali katika matukio ya kijamii na kidini, wakisema hatua hiyo inaimarisha uhusiano mzuri kati ya serikali na wananchi.
Baraza hilo limehitimishwa kwa dua maalum za kuliombea taifa amani, umoja na maendeleo.






0 Comments