MAAGIZO ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina yameanza kuzaa matunda ya kihistoria, baada ya thamani ya uwekezaji wa Serikali kwenye kampuni zenye hisa chache kuongezeka kutoka Sh bilioni 821 hadi kufikia Sh trilioni 1.9 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Ongezeko hilo la asilimia 156 ni kielelezo cha imani kubwa ambayo sekta binafsi imepata kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Mkurugenzi wa Mashirika ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amebainisha kuwa uamuzi huo wa kimkakati umesababisha gawio la uwekezaji kupaa kutoka Sh bilioni 58 hadi Sh bilioni 266, ikiwa ni ongezeko la asilimia 357.
Fedha hizi za gawio si tarakimu tu kwenye karatasi; ndizo zinazokwenda kujenga barabara, vituo vya afya, kusomesha watoto wetu na kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania.
Faida ya uwekezaji huu imevuka mipaka ya kifedha na kuingia kwenye ukuzaji wa rasilimali watu. Kwa mfano, kupitia ushirikiano na Kampuni ya Airtel, Watanzania 11 sasa wameajiriwa nje ya nchi katika kampuni mama, hatua inayoliongezea Taifa ujuzi wa kiwango cha kimataifa. Huu ni uthibitisho kuwa Serikali inapowekeza hisa chache, inafungua milango kwa vijana wa Kitanzania kushindana katika soko la ajira duniani.
Katika sekta ya kilimo, ushirikiano wa Serikali na Kampuni ya Sukari ya Kilombero (ambapo Serikali inamiliki 25%) umeleta mapinduzi ya moja kwa moja kwa mkulima. Kiwanda hicho sasa kimepanuka na kuongeza ununuzi wa miwa kutoka tani 600,000 hadi tani milioni 1.5. Hii ina maana kuwa fedha nyingi zaidi zinaingia kwenye mifuko ya wakulima wadogo wa miwa, hali inayoinua uchumi wa kaya na kuchochea biashara vijijini.
Pamoja na mafanikio haya ya kibiashara, Serikali imesisitiza kuwa haitaachia umiliki wa taasisi zenye maslahi ya kiusalama na kimkakati kwa Taifa. Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea kuwa na uwakilishi kwenye bodi za kampuni hizi ili kuhakikisha kila uamuzi unafanywa kwa faida ya Watanzania. Ili kuendeleza kasi hii, mkutano mkubwa wa wakurugenzi wa bodi utafanyika Arusha Machi 16-18, 2026, lengo likiwa ni kujengeana uwezo na kuhakikisha uwekezaji huu unaendelea kuwa neema kwa Taifa.

0 Comments