Katika ulimwengu wa karakana ambao mara nyingi hutawaliwa na sauti nzito za wanaume na harufu ya girisi, binti mmoja mwenye umri wa miaka 20, Zainab Hamis Ramadhani, anaanza kuandika historia mpya. Zainab, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kigamboni, amedhamiria kuthibitisha kuwa ufundi wa magari si kazi ya jinsia fulani, bali ni kazi ya moyo, akili, na uthubutu.
Kupitia ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), binti huyu sasa yupo kwenye safari ya kugeuza mapenzi yake ya tangu utotoni kuwa taaluma ya kuheshimika.
Safari ya Zainab ilianzia mkoani Dodoma, ambapo alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Kiganga na baadaye kuhitimu elimu ya sekondari katika shule ya Mnyakongo wilayani Kongwa.
Akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya wakulima, Telphena Wilson na Hamis Ramadhani, Zainab hakuogopa kuchagua njia tofauti na wenzake. Aliposikia tangazo kupitia vyombo vya habari kuhusu programu ya kukuza ujuzi, hakusita; alichagua fani ya ufundi magari (motor vehicle mechanics), kitu ambacho wengi walikiona kuwa ni kigumu kwa mwanamke, lakini kwake kilikuwa ni wito uliotoka ndani ya uvungu wa moyo wake.
Zainab anaelezea ndoto yake kwa shauku kubwa inayoweza kumuambukiza yeyote anayemsikiliza. Kwake, gari si chuma tu, bali ni kitu kinachohitaji uelewa wa kina sawa na daktari anayemfanyia mgonjwa upasuaji.
Anasema anataka kulijua kila eneo la gari kwa undani kiasi kwamba, injini ikipata hitilafu na "ikimuona" Zainab, iweze "kutishika" kwa sababu inajua imekutana na fundi mahiri.
"Nataka nifanye surgery ya gari," anasema Zainab kwa kujiamini, akisisitiza kuwa anatamani kuwa mhandisi wa magari anayeaminika na kuleta heshima kwa wanawake katika sekta hiyo.
Licha ya kuwa ndani ya mafunzo kwa miezi miwili tu, maendeleo yake ni ya kupigiwa mfano. Zainab tayari amemudu misingi muhimu ya karakana, ikiwemo masuala ya usalama kazini, ukarabati wa kinga (preventive maintenance), kazi za benchi (bench work), na ufanyaji wa huduma za kawaida za magari (service).
Kwake, changamoto za kazi hiyo hazimkatishi tamaa; badala yake, zinaongeza ari yake ya kujifunza zaidi. Hajali maneno ya wanaomshangaa, kwani anaamini kuwa mwanamke anaweza kufanya lolote lile mradi tu aweke moyo wake na bidii katika jambo hilo.
Simulizi ya Zainab ni kielelezo cha mafanikio ya dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumwinua binti wa Kitanzania kupitia elimu ya stadi za kazi.
Hakika Kutoka katika mashamba ya Kongwa hadi kwenye karakana za kisasa za Kigamboni, Zainab Hamis Ramadhani anajijenga kuwa fundi asiye na hofu, binti ambaye hivi karibuni atakuwa msaada mkubwa kwa familia yake na chachu ya mabadiliko kwa wasichana wengine nchini.
Anaamini kuwa uzoefu ni walimu bora, na kwa Zainab, kila nati anayokaza na kila injini anayofungua, ni hatua moja mbele kuelekea kuwa makenika mkubwa atakayetikisa soko la ajira.
0 Comments