Katika kuelekea mwaka wa fedha 2026/2027, mazingira ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini yanatarajiwa kupata sura mpya ya uwajibikaji baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kupitisha randama ya mpango na bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Hatua hii ni salamu tosha kwa watumiaji wa mitandao wanaotumia majukwaa hayo kwa ajili ya kuporomosha matusi na kukiuka maadili, kwani moja ya vipaumbele saba vilivyowasilishwa na Waziri Angellah Kairuki ni kutunga, kuhuisha na kusimamia utekelezaji wa miongozo inayosimamia sekta hiyo.
Kwa kuomba kuidhinishiwa matumizi ya shilingi bilioni 222.58, wizara imedhamiria kuimarisha ulinzi na usalama wa anga ya mtandao, jambo ambalo litadhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu na kuhakikisha kuwa teknolojoia inatumika kwa tija badala ya kuwa uwanja wa migogoro na kashfa.
Uwekezaji huu mkubwa haushughulikii tu nidhamu, bali unalenga kugeuza matumizi ya intaneti kuwa fursa ya kiuchumi kupitia kuimarisha miundombinu itakayowezesha utekelezaji wa uchumi wa kidijitali na kukuza biashara mtandao nchini.
Waziri Kairuki amebainisha kuwa serikali imejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuchochea ubunifu na kuimarisha ustawi wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups), hatua ambayo itawafanya vijana wengi wanaopoteza muda mitandaoni kuanza kufikiria fursa za kujiingizia kipato kupitia mifumo rasmi.
Aidha, bajeti hiyo inahusisha uimarishaji wa huduma za mawasiliano ya simu na posta kote nchini, pamoja na utekelezaji wa Programu ya Anga za Juu, ikiwa ni mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa mshindani katika nyanja za kisasa za kiteknolojia duniani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, ameipongeza wizara kwa usimamizi mzuri wa taasisi zilizo chini yake, akibainisha kuwa huduma za mawasiliano zimekuwa bora na za uhakika kwa wananchi.
Pongezi hizo ni kielelezo kuwa serikali sasa inahamia katika hatua ya kuhakikisha huduma hizi zinatumiwa kwa heshima na kufuata sheria, huku ulinzi wa anga ya mtandao ukitarajiwa kuwa mwarobaini wa tabia za kukebehi na kutukana zilizokithiri miongoni mwa watumiaji wa mitandao.
Kwa kupitishwa kwa bajeti hii, wizara inajiandaa kutengeneza mfumo wa kidijitali ambao si tu unachochea ukuaji wa uchumi, bali pia unalinda maadili ya Kitanzania na kuleta nidhamu ya matumizi ya habari kwa manufaa ya taifa zima.
0 Comments