Katika kipindi ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, kumeibuka wimbi la watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kutengeneza taharuki na kusambaza taarifa zisizo na tija kwa mustakabali wa taifa.
Hali hii imewalazimu wadau wa usalama na wataalamu wa masuala ya kijamii kutoa onyo kali dhidi ya vitendo vya uchochezi ambavyo vinalenga kurudisha nyuma juhudi za maendeleo zilizofikiwa na nchi.
Badala ya mitandao hiyo kutumika kama nyenzo ya ubunifu, kujifunza na kujenga uchumi, baadhi ya watu wameigeuza kuwa uwanja wa kupandikiza chuki na hasira miongoni mwa wananchi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa na mshikamano wa kijamii.
Mchambuzi wa masuala ya kiusalama, Bwana Richard Mabele, ameweka wazi kuwa historia ya mataifa mbalimbali duniani inaonyesha namna mitandao ya kijamii ilivyowahi kutumika kama silaha ya kuangamiza amani na utulivu. Akitolea mfano wa nchi ya Libya, ameeleza namna raia wa taifa hilo walivyoshawishiwa kupitia taarifa za uongo na chuki mtandaoni hadi wakachukua hatua zilizosababisha kuanguka kwa serikali yao na kuingia kwenye dimbwi la umaskini na machafuko yasiyoisha mpaka leo.
Hili ni somo tosha kwa Watanzania kuacha kuwafuata na kuwaamini watu wanaojificha nyuma ya kioo cha simu na kompyuta ili kuchochea ghasia huku wao wakiwa wamejificha kwenye maeneo salama.
Uzalendo wa kweli unapaswa kupimwa kwa namna mwananchi anavyoweza kuilinda na kuitetea nchi yake dhidi ya wale wanaotanguliza maslahi binafsi na uroho wa madaraka.
Kuna kundi la watu ambalo malengo yao makuu ni kuvuruga amani ili kupata mwanya wa kufaidi rasilimali za nchi, wakiamini kuwa njia pekee ya kufanikisha azma yao ni kuwagombanisha Watanzania na kuwafanya wapoteze mwelekeo wa kimaendeleo. Kila Mtanzania ana wajibu wa kuwa mstari wa mbele kumkataa mtu yeyote mwenye viashiria vya uvunjifu wa amani, kwani amani ikitoweka, gharama ya kuirejesha ni kubwa na inaweza kuchukua miongo mingi huku vizazi vikiteseka.
Serikali na mamlaka husika zinaendelea kusisitiza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA yanapaswa kuwa chanya kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa nchi.
Ni muhimu kwa vijana na watumiaji wote wa mitandao kuwa na uwezo wa kuchuja habari wanazozipokea na kutokubali kutumiwa kama daraja la kusambaza sumu ya utengano. Maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana katika mazingira ya fujo na malumbano yasiyoisha, hivyo ni wakati wa kila mwananchi kuamua kwa dhati kutumia teknolojia kwa ajili ya kujenga badala ya kubomoa, na kuwapuuza wale wote wanaoeneza chuki kwa kivuli cha uhuru wa maoni.
Hakika ulinzi wa amani ya Tanzania ni jukumu la kila mmoja wetu na si la vyombo vya ulinzi pekee. Kwa kuwakataa wachochezi na wanaojenga mambo yasiyo na maana kwa taifa, Watanzania watakuwa wamejiwekea kinga madhubuti dhidi ya maadui wa ndani na nje wanaolenga kuchelewesha maendeleo.
Ni lazima tuendelee kuilinda Tanzania yetu kwa wivu mkubwa, tukitambua kuwa umoja wetu ndiyo nguvu yetu na ndiyo siri ya mafanikio tuliyonayo leo, hivyo hatupaswi kuruhusu mpuuzi yeyote achezee tunu hii muhimu ya amani tuliyoachiwa na waasisi wa taifa hili.
0 Comments