RAIS SAMIA AHIMIZA AMANI, MAADILI NA MSHIKAMANO BARAZA LA EID

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewasihi Watanzania kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwa kuzingatia mafundisho ya vitabu vitakatifu, akisisitiza umuhimu wa kusaidiana, kuchukuliana na kupendana. 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kama mgeni rasmi katika Baraza la Eid el-Fitr kitaifa lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia ameeleza kuwa maadili ya kimungu ni msingi wa kujenga taifa imara na lenye mshikamano. 

Alihimiza wananchi kuendeleza upendo na uvumilivu ili kudumisha amani na utulivu nchini, akibainisha kuwa utulivu uliopo ni mtaji mkuu wa maendeleo unaopaswa kuthaminiwa na kila mmoja.

Katika hafla hiyo yenye kaulimbiu isemayo "Amani na maadili katika ujenzi wa jamii bora," Rais Samia amewatakia Waislamu na Watanzania wote sikukuu njema ya Eid al-Fitr, huku akitumia fursa hiyo pia kuwatakia waumini wa dini ya Kikristo Kwaresma njema. 

Kupitia ujumbe wake, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia wananchi kukamilisha ibada ya Swaumu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuomba dua, funga na sadaka zilizotolewa kwa unyenyekevu zipokelewe. 

Rais alibainisha kuwa mwaka huu Waislamu na Wakristo walipata fursa ya kufunga kwa nyakati zinazoshabihiana, jambo alilolitaja kuwa ni baraka na ishara ya kuimarisha undugu na mshikamano wa kitaifa.

Rais Samia ametoa mwito kwa wananchi kuimarisha mshikamano na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa taifa, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za migogoro. 

Alionya kuwa si kila mtu anapenda kuona Tanzania ikiendelea kuwa kisiwa cha amani, hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuilinda sifa hiyo kwa vitendo, huku akisisitiza kuwa tofauti za kiimani zinapaswa kuwa daraja la kuimarisha umoja badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko. 

Aidha, alitoa tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuchochea chuki na kusisitiza kuwa, ingawa serikali italinda uhuru wa kuabudu, uhuru huo usitumike vibaya kuvuruga mshikamano.

Vilevile, Rais amewapongeza viongozi wa dini kwa mchango wao mkubwa wa kuwa sauti ya matumaini na mwongozo wa kimaadili kwa waumini, hasa katika nyakati za changamoto. 

Katika hatua nyingine, alilipongeza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa juhudi zake za kuchangia maendeleo ya jamii, hususani mpango wa kujenga hospitali ya hadhi ya rufaa mkoani Dar es Salaam na vituo vya afya mikoani, akiahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao. 

Kuhusu uchaguzi wa Bakwata unaotarajiwa, Rais amehimiza kuwepo kwa utulivu na ustahimilivu miongoni mwa wanachama, akitaka washindi na wasioshinda washirikiane kwa mustakabali wa chombo hicho.

Post a Comment

0 Comments