TANZANIA YAINGIA KWENYE RAMANI YA DUNIA: MAGARI YA UMEME NA MAPINDUZI YA VIWANDA

Tanzania imepiga hatua nyingine kubwa katika nyanja ya ubunifu na uwekezaji kufuatia tangazo la kampuni ya DOW ELEF AUTO EV (ZERA) Limited kuanza kuagiza na kujiandaa kuzindua kiwanda cha kuunganisha magari ya umeme (Electric Vehicles - EV) hapa nchini. 

Hatua hii inaifanya kampuni hiyo kuwa ya pili nchini baada ya ile ya Kay Pee inayomilikiwa na mbunifu maarufu Masoud Kipanya ambaye yeye kampuni yake inaunda magari hayo hapa nchini. 

Uzinduzi huu, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, unaiweka Tanzania katika kundi la nchi chache duniani zinazokumbatia teknolojia ya kisasa ya usafirishaji inayotumia nishati safi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 6, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amebainisha kuwa teknolojia hii ni mkombozi wa kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja. Takwimu zinaonyesha kuwa magari ya umeme yanapunguza gharama za usafiri kwa takribani 85% ikilinganishwa na magari ya mafuta. Kwa mfano, gari la mafuta hugharimu takribani 200 TSh kwa kilomita moja, wakati gari la umeme linatumia 25 TSh pekee kwa umbali huohuo. Tofauti hii kubwa ni kichocheo tosha cha kukuza kipato cha mwananchi na kupunguza gharama za maisha.

Mapinduzi haya yanakuja wakati muafaka ambapo Tanzania inashuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme wa uhakika, jambo linalofungua milango ya uwekezaji katika vituo vya kuchaji magari (charging stations) nchi nzima. 

Mkurugenzi wa DOW ELEF, Emmanuel Kazimoto, amesisitiza kuwa lengo la muda mrefu ni kuanzisha kiwanda kamili cha kuunganisha magari hayo hapa nchini ili kutengeneza ajira kwa vijana na kuwajengea ujuzi wa kiteknolojia (tech-skills), badala ya Tanzania kuendelea kuwa mlaji wa bidhaa zilizokamilika kutoka nje pekee.

Dhamira hii ni matokeo ya mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kupitishwa kwa Mfumo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme mnamo Desemba 2024. Kwa kuweka kipaumbele kwenye nishati safi, Tanzania siyo tu inaimarisha uchumi wake wa ndani na kupunguza utegemezi wa mafuta ya nje, bali pia inashiriki kikamilifu katika mapambano ya kidunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza hewa ukaa, huku ikielekea kuwa kitovu cha teknolojia ya kijani (Green Technology) katika ukanda wa Afrika Mashariki.



Post a Comment

0 Comments