Tanzania yawasilisha hoja kimataifa uwekezaji sekta ya afya

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa hoja nzito katika jukwaa la kimataifa jijini London, Uingereza, ikitangaza utayari wake wa kushirikiana na wawekezaji wakubwa duniani katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya afya na sayansi.

Katika jukwaa hilo la uwekezaji lililoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Tanzania imebainisha dhamira yake ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya soko la ndani na lile la bara la Afrika kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, amewahakikishia washiriki wa jukwaa hilo kuwa serikali imeweka mazingira rafiki na wezeshi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Alisisitiza kuwa juhudi hizi zinaongozwa na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka kipaumbele cha kipekee katika kuimarisha usalama wa afya kupitia maendeleo ya viwanda na ushirikiano wa kimkakati na mataifa yaliyoendelea kiteknolojia.

Tanzania sasa inaiona sekta ya afya kama injini muhimu ya ukuaji wa uchumi na si huduma ya kijamii pekee, ambapo lengo ni kuhama kutoka kuwa soko la bidhaa zinazoagizwa nje na kuwa mzalishaji mkuu. 

Uzoefu uliopatikana wakati wa janga la UVIKO-19 umeifanya nchi kuona umuhimu wa kuwa na uwezo wa ndani wa kutengeneza dawa, chanjo, na vifaa tiba ili kuepuka hatari ya kukosekana kwa huduma muhimu wakati wa dharura za kidunia. Kwa sasa, Tanzania ina soko la uhakika la watu zaidi ya milioni 65, huku mageuzi ya mfumo wa bima ya afya yakitarajiwa kuongeza mahitaji ya bidhaa za afya kwa namna inayotabirika.

Mbali na soko la ndani, nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaipa nchi faida ya kipekee ya kuhudumia soko kubwa la kikanda. 

Ili kurahisisha uwekezaji huu, Tanzania  imeanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (PIAT) na kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi kama vile Mloganzila na Kibaha. Maeneo haya yametengwa mahususi kwa ajili ya viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kurahisisha upatikanaji wa miundombinu na vibali kwa wawekezaji.

Serikali imesema inakaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika uzalishaji, mifumo ya uchunguzi wa magonjwa, usambazaji, na utafiti. 


Post a Comment

0 Comments