TUME YA MARIDHIANO YAWEKA HISTORIA, VIZABIZABINA SASA KUNYAMAZA KWA AIBU!

WAKATI wapiga kelele na vizabizabina wakihangaika mitaani kutaka kuchafua taswira ya nchi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais shupavu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imezidi kudhihirisha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa. 

Wachambuzi wa mambo na wasomi nguli nchini wameeleza matumaini makubwa kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Uchaguzi wa 2025, wakisema ni hatua ya kijasiri inayolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa kuelekea Dira ya 2050.

Uamuzi huu wa Rais Samia kuunda tume hiyo kisheria chini ya Sura ya 32, umepokewa kama "kibao cha uso" kwa wale wote waliokuwa wanavizia mifarakano. 
Mhadhiri wa UDSM, Dk. Richard Mbunda, amebainisha kuwa tume hii si ya mchezo; inachimba mizizi ya yaliyotokea ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha amani na utulivu—mtaji ambao ndio injini ya maendeleo ya kishindo ya Awamu ya Sita.

Huku nchi ikielekea kwenye Dira ya 2050, wachambuzi kama Dk. Paul Loisulie wa UDOM wamepongeza juhudi hizi za kuziba nyufa za kutoaminiana. Ameilinganisha hatua hii na busara zilizotumika Zanzibar na Kenya, akisisitiza kuwa Serikali ya Mama Samia imekuwa mstari wa mbele kutafuta tiba ya kudumu badala ya kuficha matatizo chini ya kapeti. 

Huu ni ushahidi mwingine kwamba Serikali hii haina muda wa majungu, bali imejikita katika kuponya vidonda na kujenga uzalendo.

Tume hiyo, ambayo ilianza kazi Novemba 20 mwaka jana, sasa inakaribia kukamilisha ripoti yake ifikapo Aprili 3, 2026. Wananchi wazalendo wameonekana kuwa na shauku kubwa ya kuona ripoti hii ikizika rasmi uhasama na kutoa mwongozo wa namna ya kulinda amani yetu.

Wakati vizabizabina wakijaribu kupotosha kila hatua ya serikali, ukweli unabaki kuwa hakuna mbadala wa amani katika kuleta maendeleo. 

Rais Samia amedhihirisha kuwa yeye ni kiongozi wa wote—anayesikiliza, anayechunguza, na anayechukua hatua za kisheria kuweka mambo sawa.

Kwa hatua hii, Tanzania sasa inapita kwenye tanuru la kusafisha siasa zake ili ifikapo 2050, tuwe na taifa lenye umoja wa chuma, uchumi imara, na jamii inayojivunia uzalendo wake. 

Wale wote waliokuwa wanatabiri mabaya, sasa ni wakati wao wa kukaa kimya na kushuhudia namna "Kazi Inavyoendelea" kwa vitendo!

Post a Comment

0 Comments