Kituo cha Wanawake Wajasiriamali cha Manispaa ya Kibaha kimefanikiwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania katika medani za kimataifa, baada ya bidhaa zao za batiki kupata mapokezi makubwa na kuongoza kwa mauzo kwenye maonesho ya nchi jirani.
Mwenyekiti wa kituo hicho, Dk. Magdalena Mangi, amebainisha kuwa ubora wa vitambaa wanavyotumia, ambavyo ni vizito na havichuji, umekuwa kivutio kikubwa katika maonesho yaliyofanyika nchini Burundi (2023), Sudan Kusini (2024), na hivi karibuni nchini Kenya (2025).
Mafanikio hayo yamekijengea kituo hicho soko thabiti miongoni mwa watu binafsi na taasisi mbalimbali, hali inayothibitisha kuwa ubunifu na ujasiriamali ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto ya ajira nchini.
Kutokana na ongezeko la mahitaji katika masoko ya nje na ndani, wajasiriamali hao wamejipanga kupiga hatua kutoka uzalishaji wa mikono kuelekea uanzishaji wa kiwanda cha kisasa cha batiki.
Dk. Magdalena ameeleza kuwa matumizi ya mashine yatasaidia kuongeza maradufu ubora na wingi wa bidhaa hizo ili kukidhi ushindani wa soko la kimataifa. Lengo la kituo hicho ni kuhakikisha batiki za Tanzania zinatambulika kama bidhaa zenye hadhi ya juu, huku wakipanga kutumia nguvu kubwa zaidi katika kujitangaza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wengi zaidi duniani kote.
Licha ya mafanikio hayo, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa mtaji na ufinyu wa eneo la kufanyia kazi, jambo linalowalazimu baadhi ya wanachama kuzalishia bidhaa hizo nyumbani.
Hadi sasa, wajasiriamali hao wanaendelea kurejesha mkopo wa Shilingi milioni 40 walioupata kutoka halmashauri, huku wakitafuta rasilimali fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda.
Wajasiriamali hao wameitoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezesha na kutoa mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na mamlaka za mitaa, ambayo imekuwa mhimili mkuu wa kukuza biashara zao. Kupitia uwezeshaji huo, Kituo cha Wanawake Wajasiriamali Kibaha kinajipambanua kama mfano wa kuigwa katika jitihada za serikali za kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani.
0 Comments