Wakati baadhi ya watu wenye nia ovu wakijaribu kupaka matope jitihada za serikali kupitia majukwaa ya mitandaoni, takwimu za kiuchumi za hivi karibuni zimekuja kama jibu la mapigo likithibitisha kuwa kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji.
Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu mwenendo wa uchumi kwa mwezi Februari 2026, inaonesha picha ya nchi inayopaa kwa kasi, huku sekta muhimu kama utalii, madini, na viwanda zikirekodi mafanikio makubwa ambayo hayawezi kufichwa na propaganda za kisiasa.
Hali hii inathibitisha kuwa Tanzania inaendelea kusonga mbele kwa kishindo, huku ikitandika misingi imara ya kiuchumi inayowagusa wananchi wa ngazi zote kupitia ukuaji wa mapato na fursa za mikopo.
Sekta ya utalii imeendelea kuwa mhimili mkuu wa fedha za kigeni baada ya kurekodi mapato ya dola za Marekani milioni 3,969.6 katika mwaka ulioishia Januari 2026, ikiwa ni ongezeko kutoka dola milioni 3,933.7 za kipindi kama hicho mwaka jana. Ongezeko hili la mapato lilienda sambamba na ukuaji wa idadi ya watalii kwa asilimia 6.1, ambapo jumla ya watalii 2,289,867 walitembelea vivutio vya nchi yetu, hali inayodhihirisha kuwa juhudi za kutangaza utalii zinaendelea kuzaa matunda ya dhahabu.
Ukuaji huu wa mapato ya huduma haukuishia kwenye utalii pekee, bali ulichangiwa pia na shughuli za usafirishaji, jambo linaloifanya sekta ya huduma kuwa injini muhimu katika kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa na huduma ambayo kwa ujumla yaliongezeka kwa asilimia 12.7.
Katika upande wa madini, dhahabu imeendelea kung'ara baada ya mauzo yake nje ya nchi kupaa kwa asilimia 39.3, yakifikia dola za Marekani milioni 4,900.7 ikilinganishwa na dola milioni 3,517.5 za mwaka uliopita.
Ongezeko hili la kihistoria limechangiwa na mchanganyiko wa bei nzuri katika soko la dunia na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani, jambo linaloashiria usimamizi madhubuti wa rasilimali za taifa.
Sambamba na mafanikio hayo, bidhaa za viwandani nazo hazikuachwa nyuma kwani mauzo yake nje yaliongezeka kwa asilimia 28.9, yakichangiwa zaidi na mahitaji makubwa kutoka nchi jirani, hali inayothibitisha kuwa viwanda vya Tanzania sasa vinazalisha kwa ajili ya soko la kikanda.
Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia mfumo wa kifedha umeshika kasi, ambapo taarifa ya BoT inaonesha kuwa mikopo katika shughuli za uchimbaji madini na mawe ilirekodi ukuaji wa juu wa asilimia 91.4. Ongezeko hili linatokana na hatua za makusudi za serikali kuboresha sekta ya madini na kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kupitia matumizi ya dhamana zinazoendana na mahitaji yao halisi. Pia, shughuli za biashara, usafirishaji, na mawasiliano nazo zilipata msukumo mkubwa wa mikopo, huku shughuli binafsi za wajasiriamali wadogo sana na wa kati zikichukua sehemu kubwa ya mikopo yote ya sekta binafsi kwa asilimia 35.6, ikifuatiwa na biashara na kilimo.
Licha ya ukuaji huu wa kasi wa kiuchumi, serikali imefanikiwa kudhibiti hali ya maisha ya mwananchi kwa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki kuwa tulivu ndani ya wigo wa kitaifa wa asilimia 3 hadi 5.
Kwa mwezi Januari 2026, mfumuko wa bei wa chakula ulishuka hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 6.7 mwezi Desemba 2025, hatua ambayo inaendana na vigezo vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Uthabiti huu wa bei za bidhaa sokoni ni kielelezo tosha kuwa mipango ya serikali haishia kwenye makaratasi tu, bali inaleta nafuu ya maisha kwa wananchi huku taifa likiendelea kuchanja mbuga kuelekea uchumi wa kati na wa juu.
Ukweli wa takwimu hizi kutoka Benki Kuu unadhihirisha kuwa jitihada za kuhujumu taswira ya nchi mitandaoni ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Tanzania inasonga mbele ikiwa imejizatiti kwenye sekta za kimkakati kama madini, utalii, na kilimo, huku ikitengeneza mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo kupitia mikopo na miundombinu.
Wakati wanafiki wakihangaika kutafuta dosari ambazo hazipo, taifa linaendelea kushuhudia mapinduzi ya kiuchumi yanayozalisha ajira na kuleta fedha za kigeni, ikithibitisha kuwa safari ya maendeleo ya Tanzania haina breki.
0 Comments