HOBOKELA SWILLA: Amani huleta tabasamu

Na Gordon Kalulunga, Mbeya

MJASIRIAMALI na mdau wa maendeleo nchini, Hobokela Swilla, ametoa mwito kwa Watanzania kuendelea kuilinda na kuistawisha amani iliyopo, akisisitiza kuwa utulivu ndio msingi mkuu wa furaha na tabasamu kwa mwananchi mmoja mmoja.

Akitoa maoni yake kuhusu umuhimu wa utulivu wa kitaifa, Swilla alisema kuwa matukio ya mivutano yaliyoshuhudiwa mnamo Oktoba 2025 yanapaswa kubaki kama somo kubwa na lisilostahili kurejelewa tena, kutokana na changamoto na shida nyingi zilizowapata wananchi wakati huo

Swilla amebainisha kuwa amani ni tunda la maelewano na kusikilizana, hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuwa na utaratibu wa kusikiliza maoni ya wananchi kwa upana zaidi. 
Alieleza kuwa hatua ya Serikali kuwa na "masikio marefu" na kuzingatia maoni ya umma husaidia kupunguza manung’uniko.

“Amani na utulivu huleta tabasamu. Ni wajibu wetu sote kuilinda kwa gharama yoyote. Lakini pia, pale wananchi wanapotoa maoni yao, ni vyema yakasikilizwa kwa staha na kutafutiwa ufumbuzi wa kibusara ,” alisema Swilla.

Aidha, alihitimisha kwa kusema kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijasiriamali hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira tulivu, hivyo akawataka Watanzania kuwa wamoja katika kulinda tunu hiyo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments