Mjumbe wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mkuu mstaafu Profesa Ibrahim Juma, amebainisha kuwa kuundwa kwa tume hiyo ni ujumbe tosha kwa jumuiya ya kimataifa kwamba Tanzania ina uwezo na utashi wa kushughulikia changamoto zake za ndani na kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 14, Profesa Juma alieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha uwazi wa nchi na uwepo wa taasisi imara zinazoweza kusimamia masuala makubwa kwa weledi wa hali ya juu.
Alisisitiza kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, anatumia uzoefu wake mpana wa kimataifa kuwaongoza wajumbe ili wasitegemee sheria za Tanzania pekee, bali wazingatie viwango vya kimataifa wakati wa kupanga vigezo vya ripoti yao
Jaji Chande, ambaye amekuwa mjumbe wa tume mbalimbali duniani zikiwemo za kuchunguza kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa na migogoro ya Darfur na Ethiopia, anahakikisha kuwa taarifa itakayotolewa inapimwa kwa vigezo vya kidunia, alisema Profesa Juma.
Aidha, Profesa Juma alionyesha imani kubwa kwa timu ya wataalamu wa kitanzania, wakiwemo wa masuala ya video na mitandao, ambao wamekuwa wakitumika katika tume mbalimbali duniani.
Alibainisha kuwa tume imetembelea maeneo yote yaliyokumbwa na migogoro na kuzungumza na wahusika wote, wakiwemo waliofiwa na waliopotelewa na ndugu zao, ambao wamewasilisha ushahidi wa ana kwa ana na wa viapo.
Tume hiyo iliyoanza kazi Novemba 20, 2025, inatarajiwa kukamilisha majukumu yake ifikapo Aprili 24,2026

0 Comments