MAHUNDI AHIMIZA MAADILI NA UZALENDO KWA WAHITIMU

 


Na Oscar Tarimo, Dodoma

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wahitimu wa mahafali ya Kidato cha Sita katika Shule ya Wasichana Huruma jijini Dodoma kuzingatia  nidhamu, uzalendo na kutumia elimu yao kuleta maendeleo kwa taifa.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mhe. Mahundi amesema kuwa vijana ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi na wanapaswa kujiandaa vyema kwa hatua inayofuata ya maisha yao kwa kuzingatia maadili na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu ndoto zao.

 “Katika hatua mnayoingia sasa, taifa linatarajia mengi kutoka kwenu; muwe vijana wenye uzalendo wa dhati, wanaozingatia nidhamu na maadili, na kutumia elimu yenu kutatua changamoto za jamii.”Alisema Mhe Mahundi

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora kwa vijana kupitia uwekezaji katika elimu, afya na ustawi wa jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kufikia mafanikio yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Huruma, Sr. Alfonsia Aloyce, amesema mahafali hayo ni tukio muhimu kwa wanafunzi waliomaliza masomo yao na kuwataka wahitimu kuendeleza nidhamu na maadili waliyojifunza shuleni wanaporejea nyumbani na kuanza maisha mapya.

“Baada ya kuhitimu, mtaenda kuishi bila usimamizi wa walimu na walezi, hivyo ni muhimu kujisimamia na kuzingatia maadili na mafundisho mliyoyapata ili yawasaidie katika maisha yenu ya baadaye.”alisema sr.Alfonsina

Mahafali hayo yamefanyika tarehe 18 Aprili 2026 katika Shule ya Wasichana Huruma, ambapo wahitimu wa Kidato cha Sita wamehitimisha rasmi safari yao ya elimu ya sekondari na kujiandaa na hatua inayofuata ya masomo na maisha.

Post a Comment

0 Comments