Wakati baadhi ya mataifa barani Afrika yakiendelea kukumbwa na migogoro ya kisiasa na kijeshi, Tanzania imetakiwa kuwa macho na kuepuka mtego wa machafuko kwa kulinda tunu ya amani na utulivu iliyonayo.
Hali hiyo imekuja kufuatia uchambuzi wa mwenendo wa kisiasa barani humo, ambapo nchi kama Sudan, Libya na DRC zimetajwa kuwa mifano ya mataifa yaliyoingia kwenye machafuko baada ya umoja kuvunjika, jambo lililosababisha mamilioni ya wananchi kutaabika na uchumi kudidimia.
Imeelezwa kuwa amani ya Tanzania si jambo la bahati mbaya, bali ni tunda la misingi imara iliyowekwa tangu uhuru na Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, ambaye alihimiza umoja bila ubaguzi wa kabila, dini wala itikadi za kisiasa.
"Amani si jambo la kudumu bila jitihada; ni tunu inayohitaji kulindwa kwa juhudi, maarifa na dhamira ya kila mmoja, viongozi na wananchi," imeeleza sehemu ya tahadhari hiyo kwa umma.
Aidha, Watanzania wameonywa dhidi ya watu au makundi yanayoweza kuchochea vurugu kwa maslahi binafsi au ya nje, huku ikibainishwa kuwa migogoro mingi huanza kwa maneno ya chuki na upotoshaji kama ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Katika kuelekea hatua muhimu ya maridhiano, wananchi wameaswa kuwa na subira wakati taifa likisubiri Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu. Ripoti hiyo inatazamwa kama jukwaa la kutafuta ukweli na kuweka msingi wa maridhiano ya kudumu badala ya kuwa chanzo cha mgawanyiko.
Pamoja na hayo, imesisitizwa kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi na ulinzi wa rasilimali kama gesi asilia na madini, ambazo mara nyingi huwa shabaha ya "vita vya kiuchumi" kutoka kwa mataifa yenye maslahi ya ndani na nje.
Kazi ya kulinda amani imetajwa kuwa si jukumu la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika miundombinu na huduma za kijamii yanalindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

0 Comments