Katika historia ya mataifa mengi duniani, vipindi vya migogoro ya kisiasa mara nyingi huacha majeraha makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisaikolojia, jambo ambalo Tanzania ilikumbana nalo kufuatia ghasia za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Uzito wa Tume ya Rais ya Kuchunguza matukio hayo unatokana na uamuzi wa serikali kuchagua njia ya uwajibikaji, ukweli, na haki badala ya kupuuza kilichotokea au kuacha mjadala ubaki katika hisia na propaganda.
Hatua hii ya kuunda tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, imeonekana ni mwanzo muhimu wa safari ya maridhiano na uponyaji wa taifa kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa wananchi.
Uamuzi huo ulionesha aina ya uongozi unaotambua kuwa maridhiano ya kweli hayawezi kujengwa juu ya propaganda, bali yanahitaji uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane na taifa lijifunze.
Katika hotuba yake wakati wa kuwasilisha ripoti, Jaji Chande alisisitiza kuwa dhamira ya pamoja ya taifa ni kutibu majeraha na kuwajibika kila panapostahili ili kusonga mbele kwa pamoja.
Kauli hii inadhihirisha kuwa kazi ya Tume haikulenga kuongeza mgawanyiko, bali kutafuta njia ya kuponya taifa baada ya kipindi kigumu na kurejesha mshikamano wa asili wa Watanzania.
Moja ya mambo yaliyotoa uzito zaidi kwa kazi ya Tume ni ushirikishwaji mpana wa wananchi, ambapo mamia ya mashahidi, waathirika, viongozi wa dini na wataalamu walipata nafasi ya kusikilizwa. T
ume ilipokea maelfu ya ujumbe kupitia njia mbalimbali, jambo ambalo ni muhimu katika mchakato wa maridhiano kwa sababu wananchi wanapopewa nafasi ya kusikilizwa, hujenga hisia kwamba maumivu yao yanatambuliwa na taifa.
Kiwango hiki cha imani ambacho wananchi waliiweka kwa Tume kimekuwa msingi imara wa kujenga maridhiano, kikithibitisha kuwa kilio kikubwa cha waathirika ni kutambuliwa kwa sauti zao.
Aidha, ripoti hii imeweka wazi umuhimu wa ukweli kwa kutumia uchunguzi wa kisayansi na wa kidijitali kutofautisha ukweli na upotoshaji uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Tume ilionyesha mtazamo wa kipekee wa kibinadamu kwa kuupa uzito uhai wa binadamu, ikibainisha kuwa kila tukio liligusa familia, maisha, na ndoto za watu. Kwa kukiri wazi madhara ya kibinadamu ikiwemo vifo na majeraha, Tume imeweka msingi wa haki kwa waathirika huku ikisisitiza kuwa uwajibikaji unapaswa kuwa wa haki na unaofuata misingi ya sheria.
Mwisho, ripoti hii inakumbusha kuwa utambulisho wa Tanzania umejengwa juu ya amani na umoja, huku ikiongeza imani kwa jumuiya ya kimataifa na wadau wa maendeleo kuhusu utulivu wa nchi. Kupitia uamuzi wa kuunda Tume hii na kuruhusu ukweli kutafutwa kwa uwazi, serikali imeonesha ujasiri wa kukabiliana na changamoto zake kwa busara.
Huu ni mwanzo mpya unaotoa somo kuwa taifa imara si lile lisilokumbwa na changamoto, bali ni lile lenye uwezo wa kujijenga upya kupitia ukweli na maridhiano kwa faida ya vizazi vijavyo.

0 Comments