Maisha nchini Urusi ni mazuri na ya kuridhisha kwa kiasi kikubwa iwapo mtu ana nyaraka na nyaraka zote zinazohitajika kisheria, ambapo changamoto zilizopo zinakuwa ni zilezile za kawaida zinazowakabili hata raia wazawa wa nchi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jamii ya Watanzania Waishio nchini Urusi, Pascal Maubhi Gura, ambaye amekaa nchini humo kwa miaka 20 sasa baada ya kuhitimu masomo yake.
Gura, ambaye amejiriwa nchini humo kama mhandisi mtaalamu wa masuala ya nguzo na akiwa na familia ya mke na watoto wawili, anasisitiza kuwa Urusi ni nchi kubwa yenye shughuli mbalimbali na haina ubaguzi, hivyo inatoa nafasi nzuri kwa Watanzania kwenda kusaka fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.
Licha ya maisha kuwa ya kawaida na yenye kipato kizuri kinacholipa, changamoto hazikosekani katika mazingira yoyote ya ugenini. Kutokana na muktadha huo, jamii hiyo ya Watanzania yenye wanachama wapatao 300 imeweka mfumo thabiti wa umoja unaolenga kusaidiana wakati wa shida, pamoja na kuwapokea, kuwaelekeza na kuwasaidia wanafunzi na wageni wapya wanaowasili kutoka Tanzania ili waweze kuzoea mazingira kwa haraka.
Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa hakuna eneo gumu kuishi duniani, isipokuwa jambo kubwa na la msingi la kuzingatia kwa yeyote anayetaka kufanikiwa nchini Urusi ni kujifunza na kuimudu lugha ya Kirusi ambayo ndiyo ufunguo mkuu wa mawasiliano na fursa zote.
Katika hatua nyingine, ushirikiano wa karibu kati ya ubalozi na raia wa Kitanzania umetajwa kuwa nguzo kuu ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza ugenini.
Gura amempongeza na kumshukuru Balozi wa Tanzania nchini humo kwa kufanya kazi kubwa, kwani kila yanapotokea matatizo miongoni mwa Watanzania, ubalozi umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinamalizwa kwa wakati na kwa njia salama.
Malezi haya ya kidiplomasia yanawapa watanzania waliopo nchini humo amani na utulivu wa kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Moja ya changamoto kubwa ya hivi karibuni inayowakabili watanzania nchini Urusi ni upande wa kifedha, ambapo mifumo ya kifedha ya kimataifa iliyozoeleka nyumbani kupitia mataifa ya magharibi imesimama kufanya kazi kutokana na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa nchi hiyo.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Watanzania hao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu kusaidiana ili kuhakikisha maisha yanaenda bila kukwama. Jamii hiyo imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Tanzania kwa kuchukua hatua za makusudi na kuzungumza na Serikali ya Urusi ili kupata suluhu ya kudumu itakayorahisisha mifumo ya malipo na miamala ya kifedha kati ya mataifa haya mawili.
Historia ya uwepo wa Watanzania nchini Urusi ilianza kushika kasi tangu miaka ya 1960 kupitia ufadhili wa masomo uliotolewa na Umoja wa Kisovieti kwa mataifa machanga ya Afrika yaliyokuwa yakitafuta uhuru na maendeleo. Tangu kipindi hicho, maelfu ya Watanzania wamehitimu katika vyuo vikuu vya Urusi wakirudi nyumbani kuwa madaktari, wahandisi, marubani na wanasiasa wabobezi.
Katika miongo miwili ya hivi karibuni, mwelekeo umeruhusu pia wahitimu wengi wa Kitanzania kubaki na kuingia rasmi kwenye soko la ajira la Urusi au kuanzisha biashara, hatua inayosaidia kuimarisha mtandao wa uwakilishi wa kitanzania na kukuza diplomasia ya watu kwa watu kati ya nchi hizo mbili.

0 Comments