Baada ya lile tukio la wale mabinti (watoto) ambao, video yao ilisambaa mitandaoni hivi karibuni wakijinadi kuwa wamehitimu masomo sasa wanakuja mtaani kufanya vitendo vya hovyo, tayari Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ameshawaitisha kikao wanafunzi hao na wazazi wao na waalimu wao Oktoba 26, 2026 na wanafunzi hao kwa mara ya pili wamekiri ujinga wao na kuomba msamaha.
Katika hatua ingine, wako baadhi ya watu wazima wameendelea kuonyesha jinsi gani kumbe na wao wanao ujinga mkubwa zaidi kuliko hata hao watoto kwa kuendelea kusambaza video na picha zao na kuandika maneno ambayo watoto hao waliyasema na wengine kufikia hatua ya kuyafanya stika na kuzibandika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo vyombo vya usafiri.
Kifupi, huu ni udhalilishaji na kosa kisheria dhidi ya watoto ambao tabia zao hizo ni matokeo ya uwajibikaji mbovu wa dunia ya watu wazima kwenye kulea na kukuza watoto tunaojaliwa.
Hivyo, napenda kusema kuwa, kwa baadhi ya waliofanya udhalilishaji huo nimeshawasilisha vilelezo hivyo kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta kwa hatua stahiki chini ya vyombo vyao vya kisheria. Na wengine wote ACHENI kuendelea kuwadhalilisha watoto hawa na wengine wote.
Aidha, NAONYA na KUANGALIZA kwamba, malezi ya watoto yanatuhitaji sisi sote kama jamii inayowazunguka watoto waliozaliwa na wazazi mbalimbali na siyo kutumia fursa ya visa vya ujinga wa watoto mbalimbali kuendelea kuwadhalilisha kwani, kuna watu watajikuta gerezani kwa mujibu wa sheria ya mtoto. Tubadilike na tuwalee watoto wetu kama jamii moja.
Kwenu watoto, nanyi mnalo jukumu la kuwa wasikivu na kuzingatia malezi bora mnayopewa kwenye hatua mbalimbali za makuzi yenu na siyo kuiga mambo ya hovyo kutoka kwa watu wa hovyo na kuja kuyafanya kwani, nanyi pia kwa mujibu wa sheria yenu ya mtoto kuna hatua zenu za kisheria iwapo mnageuka wavuruga utulivu kwenye jamii. Mnaona sasa mnavyofanyiwa? Watoto, msijidhalilishe, ni hatari kwa maendeleo na ustawi wenu.

0 Comments