Imesisitizwa kuwa amani ya Tanzania ni tunu ya kipekee ambayo ni lazima ilindwe na kila mwananchi kwa wivu mkubwa, kwani ndiyo msingi mkuu unaomwezesha kila mtu kutimiza wajibu wake na kupata haki zake za msingi.
Katika mazungumzo maalumu kupitia kipindi cha #DAKIKA45 ndani ya ITV, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amebainisha kuwa bila amani, hakuna maendeleo wala utulivu wa kijamii unaoweza kupatikana.
"Amani ni msingi; palipo na amani unajua wapi pa kuzitafuta haki zako na utatimiza wajibu wako. Tunahitaji amani ili mifumo ya maisha na taasisi za kutoa haki ziweze kufanya kazi vizuri," alieleza Wakili Mpanju.
Matumizi Mabaya ya Mitandao
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka kundi dogo la watu wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kusambaza lugha za uchochezi na kukejeli juhudi za kulinda utulivu wa nchi.
Katika maoni mtandaoni yaliyoambatana na kauli ya Naibu Katibu mkuu huyo imesisistizwa uzalendo wa kidijitali ambapo Kila Mtanzania anapaswa kutumia mitandao ya kijamii kujenga nchi na si kuibomoa. Aidha imeelezwa kuwa ni muhimu kupuuza na kuripoti maudhui yoyote yanayolenga kupandikiza chuki au hofu miongoni mwa jamii.
Pia inapaswa itambuliwe kwamba amani yetu haikuja kwa bahati mbaya; imejengwa kwa misingi ya umoja na mapatano. Watu wanaojaribu kuchezea amani hii wanapaswa kutambuliwa kama maadui wa maendeleo ya kila mwananchi.
Aidha ni jukumu la kila mdau wa amani kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha utulivu. Hii ni pamoja na kusaidia mamlaka kuwafichua wale wote wanaopanga njama za kuvuruga usalama wa nchi kupitia majukwaa ya kiteknolojia.
Tanzania ni Taifa Teule
Wadau mbalimbali wameendelea kupongeza juhudi za Serikali katika kuhakikisha amani inatawala. Wananchi wamehimizwa kuendelea kuwa wamoja, kushirikiana, na kuombea Taifa ili njama zozote za kuichafua Tanzania zisifanikiwe.
Amani inapotawala, kila mwananchi kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa anapata fursa ya kustawi kiuchumi na kijamii. Ni wajibu wetu sote kuilinda Tanzania yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

0 Comments