Mdau wa Maendeleo nchini Ndele Mwaselela amewataka Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya kuandika habari zitakazosaidia kutatua changamoto za wananchi ili serikali iweze kuzitatua kwa wakati.
Ndele ameyasema hayo Jijini Mbeya katika kikao maalumu cha kutathimini mahusiano ya waandishi wa habari,wananchi,vyama na serikali kwa lengo la kujenga upendo na mshikamano.
Katika hatua nyingine Mwaselela amewataka waandishi kuisaidia serikali kwa kufichua changamoto badala ya kuficha kero zinazowakabili wananchi.
Waandishi wamesema kupitia taaluma yao wanaweza kuibua changamoto lakini maisha yao yanakuwa hatarini kutoka kwa wahusika wanaolalamikiwa.
Amesema endapo Waandishi wataibua changamoto wataisaidia Serikali kuzitatua zikiwemo za afya,barabara,maji na elimu.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya Nebert Msokwa amesema wameimarisha umoja wao na kwa sasa wanawezeshana kiuchumi.
Amesema kwa kipindi cha mwaka 2025 umekuwa mwaka wenye tija licha ya kuwapoteza baadhi ya Waandishi waliofariki wakitekeleza majukumu yao.
Amesema Waandishi wamekopeshana zaidi ya shilingi milioni mia moja ambapo Waandishi wamesomesha,wamejenga,vifaa vya kazi na kununua vyombo vya usafiri.
Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na uwezo mkubwa wa kukopeshana kwa riba nafuu hali iliyowaondoa katika lindi la kuombaomba misaada kutoka kwa wadau.



0 Comments