Vurugu Sio Tiba ya Changamoto: Athari za Kiuchumi Zinatishia Maendeleo ya Taifa

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Thomas Kibwana, ametoa msisitizo mkubwa kwa Watanzania kutumia njia za amani kutatua changamoto za kijamii na kisiasa, akionya kuwa matumizi ya nguvu hufanya taifa kurudi nyuma kimaendeleo.

Akizungumza katika mdahalo wa Athari za Kiuchumi Zitokanazo na Vurugu za Chaguzi Barani Afrika uliofanyika Makumbusho ya Taifa, Kibwana alibainisha wazi: “Hatuwezi kutatua changamoto zilizopo katika jamii kwa kutumia vurugu; badala yake, tunapaswa kutatua changamoto tulizonazo kwa njia ya amani ili kuendelea mbele bila kusababisha madhara ya kiuchumi nchini.”

Kibwana alieleza kuwa changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, hasa vurugu, zimesababisha madhara makubwa, akitaja hasa uharibifu wa miundombinu ya usafiri.

Alisisitiza kuwa hali hiyo imeathiri moja kwa moja uchumi wa taifa na kusema fedha ambazo zingeweza kutumika kuleta miradi mipya ya maendeleo hulazimika kuelekezwa kwenye kurekebisha miundombinu iliyoharibika.

Aidha alisema Vurugu na uharibifu husababisha wananchi kutumia muda mwingi katika usafiri kutokana na kuharibika kwa njia, badala ya kutumia muda huo kwenye shughuli za uzalishaji mali.

“Hali hiyo inathiri uchumi wa taifa kwa kuwa fedha zinatumika kurekebisha miundombinu iliyoharibika badala ya kuleta maendeleo,” alieleza Dkt. Kibwana. Uharibifu wa miundombinu unadhoofisha uchumi wa mtu mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa.

Mchambuzi huyo alihitimisha kwa wito wa kutafakari namna sahihi ya kutatua changamoto bila kutumia vurugu, akisisitiza kuwa ustaarabu na amani ndiyo njia pekee ya kulinda mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana. Mdahalo huo ulilenga hasa kujadili namna ya kuimarisha amani iliyopo na kuifanya iwe endelevu kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Tanzania na Afrika kwa ujumla..

Post a Comment

0 Comments