Wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee na wasiojiweza Bukumbi, wilayani Misungwi mkoani Mwanza, wameishukuru Serikali kwa kuimarisha huduma za ustawi wao, wakisema hatua hiyo imeleta faraja, heshima na matumaini mapya katika maisha yao ya uzeeni.
Mwenyekiti wa Wazee kituoni hapo, Mzee John Nguku amesema wazee wanathamini jitihada Serikali za kuwapatia huduma muhimu kwa wakati.
“Kwa niaba ya wazee wenzangu, tunaishukuru Serikali kwa kutukumbuka tunaishi kwa amani, tunahudumiwa kwa heshima na tunahisi bado tuna thamani katika jamii, tunaomba uangalizi huu uendelee ili wazee wengi zaidi wanufaike maana uzee siyo mzigo bali ni neema”. amesema Mzee John
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inawatambua wazee kama tunu muhimu ya Taifa na itaendelea kuimarisha huduma za ustawi na ulinzi wao.
Mhe. Mahundi amesema pamoja na jitihada za Serikali, jamii ina wajibu wa msingi wa kuwatunza wazee, huku akiwataka vijana kutowasahau wazazi wao wanapofikia uzee na kuhakikisha wanapata upendo, heshima na msaada unaostahili.
“Nawasihi vijana na jamii kwa ujumla, msije mkawasahau wazazi wenu wanapofikia uzee. Kuwatunza wazee ni wajibu wa familia na ni sehemu ya maadili yetu ya Kitanzania, Serikali itaendelea kuhakikisha wazee wanathaminiwa, wanalindwa na wanapata huduma stahiki bila kubaguliwa. Tunazitaka familia, vijana na jamii kwa ujumla kutambua kuwa kuwajali wazee ni wajibu wa kimaadili na msingi wa ustawi wa Taifa letu” amesema Mhe. Mahundi.
Kwa upande wake, Mfawidhi wa Makazi ya Wazee na wasiojiweza Bukumbi, Vivian Kaiza amesema uangalizi wa Serikali na ushirikiano wa wadau umeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazee waliopo kituoni hapo, Makazi yanaendelea kusimamiwa kwa weledi na kujali maslahi ya wazee, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wazee wanapata huduma stahiki na kuishi kwa amani.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya Serikali katika kuimarisha ustawi wa wazee, huku jamii ikihimizwa kushirikiana na Serikali katika kuwatunza wazee ili waishi maisha yenye heshima, upendo na matumaini.









0 Comments