Katika salamu za kuaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa taswira ya matumaini kwa kuanika mafanikio ya Serikali katika kuimarisha uchumi wa taifa.
Licha ya changamoto za kidunia, Tanzania imeweza kudhibiti mfumuko wa bei, hususan wa bidhaa muhimu za chakula, huku Pato la Taifa likikua kwa asilimia 5.8. Takwimu hizi si namba tu, bali ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanyika katika sekta za kimkakati kama madini, kilimo, utalii na huduma za kifedha, jambo linalofanya Deni la Taifa kuendelea kuwa himilivu na endelevu kwa ajili ya maendeleo ya vizazi vijavyo.
Mafanikio haya ya kiuchumi ni tunda la utulivu ambao nchi yetu imekuwa nao, na ni lazima tuchukue tahadhari kubwa ili tusiyahujumu kwa kukosa subira au kurubuniwa na watu wenye nia ovu ya kuchochea mafarakano.
Maoni ya dhihaka yanayoonekana mitandaoni yanayojaribu kupuuza takwimu hizi za ukuaji ni kielelezo cha uhitaji mkubwa wa ukombozi wa fikra. Badala ya kubeza jitihada zinazofanyika, ni wakati wa Watanzania kuungana na kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta za uzalishaji ili kujikwamua kimaisha. Tukikubali kurubuniwa na sauti za uchochezi zinazotaka kututoa kwenye mstari, tutaishia kubomoa kile tulichokijenga kwa jasho na damu.
Uzoefu wa matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 unapaswa kubaki kuwa funzo la kudumu kwetu sote, hususan vijana. Hasira na vurugu siyo njia ya kutafuta haki, bali ni daraja la kuelekea kwenye uharibifu wa urithi wetu pekee ambao ni Tanzania.
Ni jukumu la kila kijana kuwa mlinzi wa amani na mshikamano, akijitenga na makundi yanayopandikiza chuki na kufuata mikumbo isiyo na tija. Kila hatua tunayochukua kuanzia sasa iwe na lengo la kuijenga Tanzania tunayotaka kuiona kesho, tukiweka mbele busara na mazungumzo katika kutatua changamoto zetu badala ya kutafuta visasi au kuingia kwenye mtego wa taharuki ya kisaikolojia.
Viongozi wa dini na taasisi za kijamii mnao mchango mkubwa katika safari hii ya kuelekea 2026 kuwa mwaka wa mafanikio na ustawi. Nyie ndio taa inayopaswa kumulika giza la hofu na kukata tamaa linalojaribu kutandika mioyo ya wananchi.
Tunawaomba muendelee kuwa daraja la upatanisho na nguzo ya maridhiano, mkifundisha maadili na kuimarisha welezi wa kiroho miongoni mwa jamii. Tanzania ni nyumba yetu sote na hatuna nyingine; tuilinde, tuiheshimu, na tuchangie kuifanya iwe mahali pa amani, utulivu, na ustawi wa kudumu kwa kila mmoja wetu.

0 Comments