Tanzania imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa kufuatia ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ambayo imeweka mkazo katika uponyaji wa taifa badala ya kulipiza kisasi.
Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, imebainisha kuwa dhamira kuu ya uchunguzi huo ilikuwa ni kutibu majeraha yaliyotokana na ghasia za uchaguzi na kusaidia taifa kusonga mbele kwa umoja.
Katika mazingira ambayo mara nyingi huibua sauti za hasira na malalamiko, msimamo wa Tume wa kuzingatia haki ya mpito unaonekana kuwa nguzo muhimu ya kurejesha imani miongoni mwa Watanzania na kuhakikisha kuwa tofauti za kisiasa hazigeuki kuwa chuki za kudumu.
Uadilifu wa mchakato huo umejikita katika kutambua maumivu ya waathirika, ikiwamo vifo na majeraha, huku ikisisitizwa kuwa uponyaji wa kweli huanza kwa kuthamini utu na kuwajibika kwa mujibu wa sheria pasipo upendeleo.
Tume imeweka wazi kuwa mustakabali wa Tanzania unategemea uwezo wa wananchi wake kujifunza kutokana na makosa ya nyuma na kuchagua njia ya maridhiano ambayo inazuia mzunguko wa lawama.
Kwa kuangalia mizizi ya matatizo ya kijamii na kiuchumi yaliyochochea ghasia, taifa sasa linapewa fursa ya kujenga mshikamano mpya unaozingatia maslahi mapana ya nchi, huku likiepuka kurithisha vizazi vijavyo mbegu za mgawanyiko, jambo ambalo ni msingi wa amani ya kudumu.

0 Comments