KATIKA mchakato wa kuitafuta kesho ya Tanzania iliyojaa amani, Ripoti ya Jaji Chande imetoa mwongozo wa namna gani kila mdau anapaswa kuwajibika. Moja ya maeneo nyeti yaliyoguswa ni ushiriki wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) katika kuchagiza au kutuliza ghasia.
Wadau walioshiriki kikamilifu katika mahojiano na tume, akiwemo Baby Madaha kwa upande wa wakurugenzi wa NGOs, wameeleza kuwa ripoti hii ni jibu la maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na wananchi kuanzia vyanzo vya vurugu hadi athari zake.
Sababu kubwa iliyofanya Tanzania ihitaji tume ya uchunguzi baada ya uchaguzi wa mwaka 2025 ni kwamba taifa lilihitaji ukweli, uwajibikaji na matumaini mapya.
Katika nyakati za migogoro, jamii haiwezi kujenga mustakabali imara kwa kuficha matatizo. Badala yake, maendeleo ya kweli huanzia pale taifa linapokuwa tayari kukabiliana na changamoto zake kwa uwazi, kusikiliza wananchi wake na kujifunza kutokana na yaliyopita.
Jukumu kuu la tume lilikuwa kutafuta ukweli kwa maslahi ya taifa, na ripoti hiyo imebainisha wazi kuwa baadhi ya vyanzo lazima viwajibike kwa kile kilichochagizwa.
Jaji Chande katika ripoti yake alisisitiza umuhimu wa kujifunza kutokana na yaliyotokea badala ya kubaki katika lawama. Alisema: “Ripoti tunayoiwasilisha kwako leo na mapendekezo yaliyomo yanabeba dhamira ya pamoja ya taifa ya kutibu majeraha, kuwajibika kila panapostahili lakini muhimu zaidi kujifunza na kusonga mbele.”
Hii inaashiria kuwa uponyaji wa taifa hautatokana na adhabu pekee, bali na mabadiliko ya kitaasisi na kifikra. Mchakato wa kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali ulikuwa moja ya nguzo kuu za tume hii. Katika kipindi cha migogoro, wananchi wengi hujihisi kutengwa, hivyo jukwaa la tume lilitumika kama sehemu ya maungamo na maridhiano.
Ushirikishwaji huo mpana ulihusisha maelfu ya wananchi kupitia njia mbalimbali za kisasa na za asili, kuanzia barua pepe hadi ushahidi wa ana kwa ana. Hii inaonesha kwamba serikali ya awamu ya sita ilitambua mapema kuwa utulivu wa kudumu hauji kwa kutoa matamko ya kijeshi, bali kwa kutoa nafasi kwa ukweli usemwe na misingi ya sheria itumike.
Kwa Tanzania, tume hii imekuwa mfano wa namna taasisi za uwajibikaji zinavyoweza kusaidia kuimarisha demokrasia. Kupitia mchakato wake, wananchi walipata nafasi ya kusikilizwa, ukweli ukatafutwa kwa kutumia ushahidi na taifa likaanza mjadala mpana kuhusu namna ya kulinda amani, haki na mshikamano wa kitaifa. Mwisho, somo kubwa ambalo tume hii imeiachia Tanzania ni kwamba, amani ni tunda la haki na uwazi, na bila mchakato wa kusemana ukweli na kuwajibika, kesho ya taifa inabaki shakani. Hilo ndilo somo kubwa ambalo tume hii imeiachia Tanzania.

0 Comments