MAHUNDI: UTU WA TAIFA HUPIMWA KWA NAMNA LINAVYOWAJALI WAZEE WAKE

Na Jackline Minja WMJWM Bukoba, Kagera

Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wazee nchini wanapata huduma bora na stahiki kwa kuimarisha makazi ya wazee, huduma za afya pamoja na mazingira salama yanayolinda utu na heshima yao.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, alipofanya ziara ya kutembelea Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kiilima yaliyopo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma, kusikiliza changamoto pamoja na kuhimiza maboresho ya ustawi wa wazee.

 Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa wazee ili kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama, yenye heshima na yanayokidhi mahitaji yao ya msingi, ikiwemo huduma za afya, lishe, malazi na huduma za kijamii kwani Serikali inatambua mchango mkubwa wa wazee katika kujenga Taifa, hivyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha huduma zinazotolewa katika makazi ya wazee nchini.

 “Hakuna jamii inayoweza kujivunia maendeleo ikiwa haiwajali wazee wake hivyo Wizara inaendelea kutekeleza maboresho mbalimbali ya Makazi ya Wazee nchini kupitia uboreshaji wa miundombinu na huduma muhimu kwa kuwa Wazee ni hazina ya Taifa letu ni wajibu wetu kuhakikisha wanapata huduma stahiki na wanaishi katika mazingira salama na yenye heshima" amesema Naibu Waziri  Mahundi.

Awali akiwasilisha taarifa ya makazi hayo,  Afisa Mfawidhi  wa Makazi hayo Gladness Rwiza amesema  kituo hicho ni miongoni mwa makazi 13 yanayomilikiwa na Serikali kupitia Wizara kwa sasa kinahudumia wazee 17, wakiwemo wanaume 13 na wanawake wanne ambapo Makazi hayo yanatoa huduma za malazi, chakula, matibabu, mavazi, ushauri nasaha, huduma za kiroho pamoja na ulinzi kwa wazee na wasiojiweza huku wakianzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, amesema Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na Wizara kuhakikisha Makazi ya Wazee Kiilima yanapata huduma zote muhimu kwa wakati, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, ulinzi na mazingira bora ya kuishi.

Naye Mbunge wa Bukoba Mjini , Mhe. Mhandisi Jonston Mutasingwa, akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika ustawi wa wazee na makundi maalum, amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi walio katika mazingira hatarishi wanapata huduma bora na stahiki.

Post a Comment

0 Comments