Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa kwa umma likieleza kuwa hali ya usalama nchini ni shwari kutokana na ushirikiano uliopo kati ya wananchi, wadau na vyombo vya ulinzi na usalama.
Pamoja na utulivu huo, jeshi hilo limebainisha kuwa linaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vya watu wachache wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha kufanya maandamano ambayo hayajafuata taratibu za kiusalama na kisheria.
Baadhi ya watu wanaohusishwa na mipango hiyo tayari wameshakamatwa na uchunguzi unaendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Ufuatiliaji wa jeshi hilo umebaini kuwa watu hao wamekuwa wakihamasisha vurugu kupitia mitandao ya kijamii na klabu za majadiliano mtandaoni, wakidai kuwa safari hii hawataandamana kinyonge.
Uhamasishaji huo unajumuisha vitisho vya kuua baadhi ya viongozi na wananchi, kuchoma moto shule, kuharibu na kupora mali za umma na binafsi, pamoja na kuua askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha ili wazitumie kutekeleza mipango yao ya kuondoa amani nchini.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uhamasishaji wa aina hiyo ni viashiria tosha vya nia ya kuhatarisha usalama wa maisha na mali za Watanzania, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na haliwezi kukubalika au kuvumiliwa.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kisithubutu kufanya au kushiriki katika uhalifu huo unaohamasishwa mitandaoni, likiwatahadharisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Wakati huo huo, jeshi hilo limeihimiza jamii kujiepusha na uhalifu huo na kuepuka matumizi mabaya ya mitandao. Ili kuhakikisha usalama kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba tarehe 7 Julai 2026 na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa katika viwanja vya Sabasaba barabara ya Kilwa, ulinzi umeimarishwa nchi nzima kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi ili wananchi waweze kusherehekea na kusafiri kwa amani .
Taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, wananchi wameaswa kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwani vyombo vya ulinzi viko imara.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii kutoa taarifa mapema pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani au sheria, likisisitiza kuwa vyombo vyote vya ulinzi viko tayari wakati wote kuchukua hatua za haraka na stahiki kulinda usalama wa nchi .
0 Comments