WASIOZINGATIA AFYA YA KINYWA HATARINI KUPATA MARADHI SUGU

 


Na Gordon Kalulunga.

ILI kuyafikia Maendeleo endelevu nchini, Watanzania wametakiwa kuzingatia afya ya Kinywa na Meno kwa kuwa ndiyo ufunguo wa kuwa na siha njema.

Rai hiyo imetolewa na mtaalamu wa masuala ya afya ya Kinywa na Meno, Dk. Donna Williams- Ngirwa (pichani) wakati wa mahojiano maalum na Blog hii.

Amesema kinywa na meno ndiyo mlango wa uhai na afya bora na kwamba mtu akizembea kushughulikia afya ya kinywa anakaribisha maradhi mbalimbali yakiwemo yaliyo sugu.

Dk. Donna wa Afya Bora Complete Dentistry Ltd ya Jijini Dar Es Salaam, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kumtembelea daktari wa meno angalau mara mbili kwa mwaka.

 “Magonjwa mengi ya kinywa na meno hayajitambulishi mpaka yamefikia hatua mbaya hivyo ni vyema kuwahi kuyagundua, ili uwe na siha njema”  alisema.

 “Kuna haja ya kuanzisha kampeni ya kuelimisha umma umuhimu wa afya ya kinywa kwa kuwa ndio mlango wa afya ya Mwanadamu,”  alisema na kuongeza kwamba ili watu waone umuhimu wa kujua wanachokula na madhara yake kwani ndio msingi wa afya njema ya meno na kinywa.

 Ameeleza kwamba watu wengi hawafikirii kuhusu uhusiano uliopo kati ya afya ya kinywa na afya yao kwa ujumla, kwani kinywa ndio ukuta wa kuzuia maradhi katika mwili.

Anasema maradhi ya kinywa yanapokuwa katika hatua za mwanzo ni rahisi kutibika lakini yanapokuwa katika hatua kubwa yanakuwa changamoto.

"Mtu anapokuwa na tatizo la kinywani huongeza hatari, kwa mfano ugonjwa wa rheumatoid arologist, atherosulinosis, shinikizo la damu, ugonjwa wa Alzheimers, ugonjwa wa sukari, na matatizo wakati wa kujifungua."

Amesema watu wanaougua matatizo ya kinywani , huwa na sababu tofauti zinazoweza kusababisha magonjwa mengine.

Kwa mfano, idadi kuu ya molekuli zinazozalishwa na seli za binadamu na kusababisha uvimbe katika ufizi zinaweza kufikia viungo vingine vya mwili na kusababisha athari katika maeneo hayo.

Dk. Donna amesema kwa sasa wataalamu wa afya ya kinywa wamekuwa na vifaa vya kisasa zaidi hivyo ni rahisi kubaini matatizo kabla hayajawa sugu.

“Kwa mfano ninapofanya shughuli zangu tunafuata misingi ya kimataifa ya utoaji huduma kutokana na umuhimu wake,” alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo ina teknolojia mpya.

Dk. Donna ni mmoja wa washiriki wa awali walioanzisha Kliniki ya afya ya kinywa ya Morningside Dental Care, ya New York nchini Marekani mwaka 1995.

Ametoa rai kwamba njia nzuri ya kuwezesha afya ya kinywa na meno ni kuhakikisha kwamba unamuona daktari wa meno ili aweze kukusaidia.

Post a Comment

0 Comments