Sauti kutoka Nyikani
NA TATA GORDON KALULUNGA MWAIPUNGU
KATIKA eneo la Mbalizi watu 28 wamefariki dunia kwa ajali ya Rosa iliyokuwa inasafirisha abiria.
Iligongwa na kufinyangwa jana Tarehe 07/06/2025.
Ujenzi wa Njia 4 unaendelea Mbeya lakini eneo hatarishi ni hilo la Mlima Iwambi (Mlima wa mauti), hakuna fyekeo wala greda wanaloliona wananchi.
Haihuzunishi bali inatafakarisha kwa hasira za ndani kabisa.
Ikiwapendeza wenye maamuzi ujenzi uhamie Mlima Iwambi kutanua Barabara badala ya kupeleka Machifu na waombaji kwenye eneo ambalo linahitaji utanuzi wa Barabara tu na usimamizi wa sheria za usalama Barabarani.
Polisi wa usalama Barabarani wanafanya kazi nzuri sana kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Pia yatoke maamuzi Barabara ya mchepuko ya kupitia Seminari kutokea Mbalizi kwenda Iwambi Barabara itengenezwe vizuri zaidi ili gari ndogo zipite huko wakati michakato na mengine yakiendelea.
Ripoti ya kwanza kutolewa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kuhusu hali ya dunia katika usalama wa barabarani, watu milioni 1.3 hufa kila mwaka na wengine hupata majeraha ya kudumu.
Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takriban milioni 60.4 na inapoteza watu kadhaa kila mwaka kutokana na ajali.
Idadi si ndogo hata kidogo na hasa ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya ajali hizi zingeweza kuepukika kama serikali ingeweka mkakati mzuri wa kukabiliana na tatizo hili.
Mafunzo ya imani yanatufundisha ama kutuelekeza kuwa binadamu wote ni sawa.
Ni kuwa licha ya tofauti zetu za mali, rangi, imani, pesa, kimo, kabila nk bado tu-sawa na tunao uhai ulio sawa.
Tumejengewa tofauti kubwa sana kati ya uhai wa mtawala na uhai wa sisi watu wa nyikani. wajiitao viongozi, uhai wao umeonekana kuwa na thamani sawa na makumi, mamia na ama maelfu ya wananchi wanaowaongoza.
Kifo cha kiongozi ni kifo, lakini kifo cha mwananchi asiye kiongozi ni takwimu (hata kama wote wamekufa kwa sababu inayofanana).
Ndio maana awapo kiongozi hata shughuli za nchi zitasimama, japo ili zisimame kwa mwananchi, lazima liwe janga la kitaifa.
Na ndio maana thamani ya mwananchi wa kawaida inaonekana hasa wakati wa uchaguzi, ili waweze kuwavusha wanaotaka kuwa watawala.
Tumeshuhudia namna ambavyo watawala wa nchi mbalimbali wanavyotumia maelfu ya maisha ya wananchi wao kukinga nafasi na maisha yao.
Nalisema jambo hili kwasababu kuna siku nilidokezwa kazi za walinzi wa viongozi, sihitaji kumwaga mchele kwenye ukurasa huu.
Tatizo la ajali kwa nchi yangu ya Tanzania si tatizo la jana wala juzi. Si tatizo ambalo tunaona likipata unafuu wowote na hasa siku ama nyakati hizi ambapo wasafiri huongezeka, wenye magari kutamani pesa zaidi na wenye mamlaka ya kusimamia sheria za barabarani "Kuchuma" zaidi.
Wananchi kutamani zaidi kufika ilhali wakipuuza njia sahihi za kuwafikisha huko nk. Yote juu ya yote, nyakati hizi usalama kupuuzwa na akili kuwekwa kwenye pesa na muda.
Kuna ajali iliwahi kutokea kule mkoani Mara, iliyohusisha magari mawili ya abiria na watu zaidi ya 35 kupoteza maisha, Waziri wangu wa wakati ule Dr. Harrison Mwakyembe, alitoa tamko la kuyafungia makampuni ya mabasi hayo na kutangaza kuwepo msako wa ukaguzi wa vyeti vya madereva na leseni zao..
Kwa baadhi ya sisi watu wa Nyikani haikutuingii akilini kama hiyo ni dawa, vyeti wanavyo, leseni wanazo, tena nzuri, lakini ukaguzi wa magari je upo vizuri? Au magari mengi yanapendeza kutokana na uzuri wa rangi kama makaburi ili hali ndani ya kaburi kuna maiti?
Imekuwa kawaida sasa kwa serikali yetu, kutoonyesha kuwa na mikakati madhubuti ya kupunguza na pengine kufuta ajali za kizembe, bali kinakachofuata ni salamu za rambirambi toka kwa viongozi.
Niseme wazi kuwa, tumechoshwa na salamu za rambirambi za ajali zitupatazo. Kinachokera zaidi ni kwamba salamu nyingi zinaambatana na onyo kali huku watendaji wakitakiwa kuhakikisha ajali zinapungua.
Lakini hakuna tofauti. Kwenye salaam zake za mwanzoni mwa mwaka 2009, Rais Jakaya Kikwete alisema "hatuwezi kuvumilia kutokea kwa ajali hizi wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria za usalama barabarani zipo.
Tufanye jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wetu kupunguza kwa kiwango kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo zimeshapoteza maisha ya wenzetu wengi"
Kupitia Baraza la mawaziri la Rais Jakaya Kikwete, niliwahi kumuomba mmoja wa mawaziri, ajitokeze na kuwa wa kwanza kuwa kukabiliana kikamilifu na suala la ajali, na aorodheshe atatenda nini? Vipi na kufikia lini.
"Ni nani atakayechukua jukumu la kushughulikia kuzuia ajali? Je! Ni Wizara ya Ujenzi (Barabara na Uwanja wa Ndege), Wizara ya Uchukuzi (Reli, Bandari, Usafiri Majini) ama Wizara ya Usalama wa Raia? Ama ni wizara gani?)"
Bila kuwa na mikakati inayofaa na endelevu na kutegemea tochi za trafiki wa Iringa, tunasubiri mvua za ajali ambazo hata tukipona, hatutakuwa kama tulivyokuwa awali.
Hili linanifanya niamini kuwa serikali haioni tatizo la ajali kwa waTanzania mpaka pale litakapowahusisha viongozi, na ndio maana sasa nawatakia viongozi wapate ajali kama zetu ili watatue tatizo letu na kuokoa maisha yetu.

0 Comments