VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UMEME KILA KONA, ADUI WA AMANI WAUMBUKA

TANZANIA imeingia katika ukurasa mpya wa maendeleo baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusaini mikataba ya kihistoria yenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini kote.

Tukio hilo lililofanyika Januari 17, 2026 katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, limetajwa kuwa ni msumari wa mwisho kwa wale wanaohubiri ukata na hadaa, huku likifungua milango ya uchumi kwa vijana kuanzia ngazi ya kitongoji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka vijana kutoendelea kuzubaa na badala yake kutumia umeme huo kuanzisha miradi ya kiuchumi maeneo ya vijijini badala ya kukimbilia mijini kusaka fursa.

“Tunaamini sasa vijana watabaki vijijini kufanya shughuli zao. Umeme huu ni wa matumizi ya kiuchumi. Dodoma pekee, kata zote 209 na vijiji 564 vimeshafikiwa na umeme, na sasa tunaingia kwenye vitongoji vilivyobaki,” alisema Senyamule.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesisitiza kuwa upatikanaji wa umeme vitongojini umepanda hadi asilimia 78 mwaka huu, kutoka asilimia 65 mwaka 2025. Amewaagiza wakandarasi kuhakikisha taasisi za umma kama shule na zahanati zinaunganishwa bila kukosa.

Katika hatua ya kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kwa Mhandisi Adam Chambua, limewapa wananchi mbinu ya kupunguza gharama.

"Siyo lazima kufanya wiring nyumba nzima. Unaweza kufanya wiring chumba kimoja tu na sisi tutakuwekea umeme ili uanze kunufaika na huduma hii kwa gharama nafuu," alisema Chambua, huku akiongeza kuwa shirika hilo sasa linahamia kwenye matumizi ya nguzo za zege ili kuimarisha miundombinu.

Post a Comment

0 Comments