DED ERICA YEGELLA APONGEZWA KWA KUIMARISHA MAWASILIANO NA WATUMISHI

Tume ya Utumishi wa Umma imempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica E Yegella (Kulia), kwa juhudi zake za kuimarisha mawasiliano na watumishi kupitia vikao vya mara kwa mara.

Pongezi hizo zimetolewa na Jaji (MST) Hamisa Hamis Kalombola alipokutana na watumishi wa Halmashauri hiyo katika kikao kilichofanyika leo Septemba 8,2025 katika ukumbi wa Halmashauri Makao Makuu.

Jaji Kalombola alisema kuwa hatua ya DED Erica kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watumishi wake ni jambo la kuigwa, kwani linaongeza uwazi, mshikamano, na utatuzi wa changamoto kazini.

"Mkurugenzi nakupongeza sana kwa hatua hii ya kuweka vikao mara kwa mara na watumishi. Hii inasaidia sana, kuliko kumzuia mtu kutoa dukuduku zake unaweza kutengeneza bomu. Kwa kweli unastahili pongezi," alisema Jaji Kalombola.

Aidha, alieleza kufurahishwa na hali ya mshikamano aliyoiona miongoni mwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, na kuwataka waendelee kushirikiana kwa maslahi ya umma.

Kwa upande wao, watumishi walipata nafasi ya kuzungumza na waliishukuru Tume ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea halmashauri hiyo na kuwapa elimu juu ya majukumu ya Tume. Walisema elimu hiyo imewasaidia kuelewa haki na wajibu wao kama watumishi wa umma.

Vilevile, walimpongeza DED Erica kwa kuwaongoza kwa ukaribu, kuwasikiliza na kufanyia kazi changamoto zao, hatua waliyoitaja kuwa imeongeza morali kazini na kuleta mafanikio ya kiutendaji ndani ya Halmashauri.

Tume hiyo imesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya wazi na kusikilizana kati ya viongozi na watumishi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments