AMANI YA TANZANIA DHAMANA KWA VIJANA

Katika viunga vya Soko la Uyaoni, Maili Moja, na mitaa ya Simbani mkoani Pwani, sauti za wananchi zinatoa mwangwi mmoja: Amani ya Tanzania si jambo la bahati mbaya, bali ni tunda la mshikamano na uvumilivu. 

Kupitia maoni ya wadau hawa wa Kibaha, tunapata picha ya kile kinachoifanya nchi yetu kusimama imara katikati ya misukosuko ya dunia.

Kwa wakazi wa Pwani, amani ni zaidi ya neno; ni vazi ambalo Watanzania wamejivika kama jadi yao. Mwenyekiti wa Mtaa wa Simbani, Nasra Madenge, anasisitiza kuwa utulivu ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Bila mshikamano na utii kwa maelekezo ya viongozi wetu, maendeleo tunayoyatafuta yatabaki kuwa ndoto. Uvumilivu wa mwananchi mmoja mmoja ndio unaojenga ukuta imara wa usalama wa taifa letu.

Nguvu ya taifa lolote ipo mikononi mwa vijana, lakini nguvu hiyo inaweza kuwa silaha ya ujenzi au uharibifu. Isaya Lwinga, mfanyabiashara wa soko la Uyaoni, anatoa wito mzito kwa vijana: "Amani yetu ndiyo silaha yetu." Anawakumbusha vijana kuwa wao ndio walengwa wakuu wa wanaotaka kuvuruga utulivu, hivyo wanapaswa kukataa kutumika kama vyombo vya uvunjifu wa amani. Katika mikono ya kijana mwenye jitihada, amani inatafsiriwa kuwa fursa ya kufanya kazi na kujipatia kipato bila hofu.

Katika kumkabili adui anayetaka kuivuruga nchi, imani na mshikamano wa kijamii ni muhimu. Cletus Kasanga, mfanyabiashara mwingine kutoka Uyaoni, anaamini kuwa kumcha Mungu ni kinga dhidi ya "wabaya" wanaovizia ustawi wa nchi yetu. Anasititiza kuwa mshikamano si chaguo, bali ni kitu tunachopaswa "kukumbatia" kwa nguvu zote ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.

Ujumbe kutoka Kibaha ni wa wazi, Amani ikitoweka, kila kitu kinatoweka. Ni jukumu la kila mfanyabiashara, kila kiongozi wa mtaa, na kila kijana kuhakikisha kuwa "mishale ya mwanga" ya maendeleo inaendelea kuangaza Tanzania kupitia kulinda amani, mshikamano, na utulivu wa kweli.

Post a Comment

0 Comments