Msigwa aliwataka waandishi kutumia majukwaa yao kutoa habari chanya (Positive Narrative) kuhusu utalii, utamaduni, na diplomasia ya kidijitali ili kupambana na habari potofu zinazojaribu kuichafua Tanzania.
"Msiishi kinyonge. Kuna mitandao inayopanga kuichafua Tanzania, nanyi msiikubalie, jibuni kwa kuandika mema ya nchi yenu," alisisitiza Msigwa huku akiwataka waandishi kujenga mshikamano na kutokubali kudhalilishwa na vyombo vya nje.
Kwa upande mwingine, Dkt. Jabiri Bakari wa TCRA alifafanua kuhusu changamoto ya kufungwa kwa baadhi ya mitandao kama X na TikTok.
Alisema kuwa Serikali wakati mwingine hulazimika kuchukua hatua hizo pale wamiliki wa mitandao ya kimataifa wanapokataa kuondoa maudhui yanayovunja sheria za nchi na kuhatarisha usalama, huku akibainisha kuwa sera za kampuni hizo mara nyingi hazizingatii maadili ya kitaifa ya Tanzania.
Kauli hizo zinatoka wakati Waandishi wa habari nchini Tanzania wameendelea kuandika historia kwa kuonyesha msimamo thabiti dhidi ya ajenda za kigeni zinazolenga kuibua mpasuko nchini.
Kupitia kalamu zao, wamehakikisha kuwa mshikamano na upendo unaoifanya Tanzania kuwa ya kipekee unalindwa kwa gharama yoyote.
Victoria Kavishe wa Dar es Salaam anasema kuwa amani ndiyo nguzo inayowezesha watu kufanya kazi na kulea familia bila hofu, na waandishi wamekuwa walinzi wa nguzo hiyo kwa kukataa kuandika habari za uchochezi.
Dkt. Ayub Rioba Chacha, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, amewahi kusisitiza kuwa uadilifu ni kufanya yaliyo sahihi kwa uaminifu bila kushawishiwa na maslahi binafsi.
Waandishi wa Tanzania wamegeuza falsafa hii kuwa muongozo wao mkuu, wakipambana na habari za kupotosha kwa kuandika ukweli uliopimwa na wenye maslahi ya kitaifa. Hii inazima kiu ya wale wanaotamani kuona nchi ikiyumba kiuchumi na kijamii kupitia propaganda za "ukoloni mambo leo" ambazo Balozi mstaafu Dkt. Mangachi Msuya amezionya kuwa zinalenga kunyonya rasilimali za nchi.
Kwa kutumia weledi wao, waandishi hawa wamejenga mazingira ambapo tofauti za kifikra zinatatuliwa kupitia mazungumzo na kusikilizana badala ya vurugu barabarani.
Katika ulimwengu wa sasa ambapo habari za uzushi (fake news) zimekuwa silaha ya kuvuruga mataifa, waandishi wa habari nchini Tanzania wamejipambanua kama majabali yaliyoiva kitaaluma kwa kutanguliza uzalendo na weledi mbele na kwa kufanya hivyo wao si dhaifu.
Uwezo wa waandishi wa Tanzania kutoingia kwenye mtego wa kuchochea vurugu unadhihirisha kuwa wao ni wasomi wanaojua vyema majukumu yao. Wametambua kuwa nguvu kazi ya vijana inapaswa kuelekezwa kwenye ujenzi wa nchi badala ya uasi. Kwa kufanya hivyo, wanahabari hawa wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa sauti ya utulivu inazidi kelele za chuki, wakithibitisha kuwa mzalendo wa kweli hupimwa kwa vitendo vya kulinda amani ya nchi yake.

0 Comments