WANANCHI WAONYA WENYE NYUMBA 'KUUZA' AMANI YA NCHI KWA TAMAA YA FEDHA

Katika kile kinachoonekana kama operesheni ya kuimarisha ulinzi wa Taifa kuanzia ngazi ya kaya, viongozi wa Serikali za Mitaa na wadau wa usalama nchini wametoa onyo kali kwa wamiliki wa nyumba wanaokubali kuhifadhi wageni wasiojulikana kwa tamaa ya fedha. Onyo hilo linakuja huku kukiwa na hofu kuwa makazi ya watu yanageuzwa kuwa "vyumba vya siri" (safe houses) kwa ajili ya kupanga njama za kihalifu na hujuma dhidi ya taswira ya Tanzania.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magole, Ilala, Gaddafi Hassani, akizungumza kwa niaba ya mtazamo mpana wa kiusalama, amesema kuwa ulinzi wa nchi si jukumu la vyombo vya dola pekee, bali unaanza na umakini wa mwenye nyumba anayempa ufunguo mtu asiyemjua.

Fedha ya Kodi dhidi ya Usaliti wa Taifa

Mwenyekiti Hassani amefichua mbinu mpya inayotumiwa na watu wenye nia ovu, wakiwemo wahalifu wa kuvuka mipaka na wachochezi wa machafuko. Amesema watu hao hupanga nyumba katika vitongoji tulivu, wakitoa kiasi kikubwa cha fedha ili "kununua" ukimya wa mwenye nyumba na kukwepa taratibu za kusajiliwa serikali za mitaa.

"Usikubali kumpa hifadhi mtu anayekupa mamilioni ya kodi lakini hataki kutoa kitambulisho wala kufika ofisi ya mtaa. Kwa kufanya hivyo, unajenga 'chimbo' la kuisaliti nchi yako. Fedha hizo ni za muda, lakini majanga ya kiusalama yakitokea, yataigharimu nchi nzima ikiwemo familia yako," alisisitiza kiongozi huyo.

Tanzania ni yetu sote. Usikubali "kuchuuzwa" kwa fedha kidogo za kodi ambazo mwisho wake ni kuingiza Taifa kwenye majanga. Uzalendo ni kumlinda jirani yako, mtaa wako, na nchi yako kwa kutomfuga adui ndani ya nyumba yako.

Ugeni kama Kivuli cha Uhujumu

Inabainika kuwa mwishoni mwa mwaka, kuna ongezeko la watu wanaohama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine au kuingia nchini kwa kivuli cha biashara na utalii, lakini lengo likiwa ni kutafuta ramani za uhalifu. Serikali imebaini kuwa baadhi ya wageni hawa hutumika na mitandao ya kidhalimu inayotaka kuchafua taswira ya Tanzania kama kisiwa cha amani.

 Wito wa "Uzalendo wa Taarifa"

Mjumbe wa Nyumba 10, Edwin Wandawanda, amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa "Afisa Usalama wa Nyumba Yake". Alisisitiza kuwa ni lazima jamii ijifunze kuwa na kutilia shaka (positive skepticism) kwa wageni wanaokuja na mitindo ya maisha isiyoeleweka.

"Tunapaswa kuelewa kuwa amani yetu inategemea usiri na umakini wetu. Ukiona mtu amepanga nyumbani kwako, hatoki mchana, ana wageni wa ajabu usiku, na hataki kujihusisha na jamii, huyo ni hatari kwa usalama wa Taifa. Toa taarifa mara moja," alisema Wandawanda.

Hatua za Kimkakati Kitaifa

Kufuatia hali hiyo, mamlaka za mitaa zimeelekezwa kushirikiana na Polisi Jamii kuhakikisha:

Uhakiki wa NIDA: Hakuna mpangaji anayeruhusiwa kuingia nyumbani bila namba au kitambulisho cha NIDA au Pasipoti halali kwa wageni.

Daftari la Wakazi: Kila mwenye nyumba ana wajibu wa kisheria kusajili wapangaji wake kwenye daftari la kijiji au mtaa.

Kufuta "Vyumba vya Siri": Nyumba yoyote itakayogundulika kuhifadhi wahalifu au watu wanaopanga njama dhidi ya nchi, mmiliki wake atachukuliwa kama mshiriki wa uovu huo (accomplice).

Post a Comment

0 Comments