ANNA LUNGUAYA AFICHUA SIRI YA KUTOKA KIMAISHA KUPITIA UBUNIFU WA MAVAZI

Ushuhuda wa Anna Lunguaya, ambaye ni Mkurugenzi wa Anna Fashion Academy, ni shule tosha kwa kijana yeyote mwenye maono makubwa lakini anayekwama kwa kisingizio cha kukosa vifaa au mtaji mkubwa. 

Anna anathibitisha kuwa siri ya mafanikio haipo katika kumiliki kila kitu tangu mwanzo, bali inatokana na uthubutu wa kuanza na kile ulichonacho huku ukikabili changamoto kwa kichwa kigumu. 

Alianza safari yake ya ushonaji kwa maono mapana licha ya upungufu wa zana za kazi, na leo amekuwa kielelezo cha namna sekta ya ubunifu inavyoweza kumwinua mtu kutoka hatua ya chini kabisa hadi kuwa mmiliki wa chuo na chapa maarufu ya mavazi nchini.

Mafanikio haya ya Anna yanaenda sambamba na msisimko mpya katika sekta ya ubunifu wa mavazi nchini Tanzania, ambapo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imebainisha kuwa hii ni nyanja inayokua kwa kasi ya ajabu. 

Kwa mujibu wa Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Thanasia Kisyeri, mahitaji makubwa ya soko yameilazimu mamlaka hiyo kuimarisha mafunzo ambapo kwa sasa vyuo vingi vya VETA nchini vinatoa taaluma hii.

Hii ni ishara tosha kuwa kijana anayetafuta ajira hapaswi kutazama kazi za maofisini pekee, bali anaweza kugeuza kipaji cha mkono kuwa biashara kubwa yenye ushindani ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Ukweli ni kwamba soko la dunia kwa sasa linatafuta bidhaa zenye utambulisho wa kipekee, jambo ambalo linampa kijana nafasi ya kujiajiri na hata kuwaajiri wengine kwa mtaji mdogo. 

Uzuri wa sekta hii ni kwamba haichagui maeneo kijiografia kwani ubunifu wako ndio unaokufanya uheshimike mjini, iwe uko mkoani Kigoma kwenye fursa za kibiashara na mataifa jirani au uko jijini Dar es Salaam. Kwa yeyote anayeona maisha yamemshinda katika nyanja nyingine, ubunifu wa mavazi unatoa nafasi ya pili ya kuanza upya na kuwa mjasiriamali anayetoa suluhisho la mavazi kwa jamii yake.

Wito uliopo kwa vijana kwa sasa ni kuacha kupoteza muda kulalamika kuhusu changamoto za ajira na badala yake wachangamkie mafunzo ya ujuzi ili waendane na soko la kisasa. Huu ni wakati wa kubadili mtazamo na kuiona sekta ya ubunifu kama mhimili wa uchumi binafsi na wa taifa kwa ujumla. Kujikita katika kujiandaa kitaaluma na kutumia fursa zilizopo mikoani, ikiwemo mikoa inayotajwa kuwa na fursa kedekede kama Kigoma, ndiyo njia pekee ya uhakika ya kumaliza kilio cha ukosefu wa ajira.

Post a Comment

0 Comments